Kamati ya Bunge yaridhishwa ujenzi Bwawa la Kizengi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:30 PM Mar 14 2025
Kamati Ya Bunge Yaridhishwa Na Ujenzi Wa Bwawa Uyui; Wizara Ya Maji Yapongezwa
Picha:Mpigapicha Wetu
Kamati Ya Bunge Yaridhishwa Na Ujenzi Wa Bwawa Uyui; Wizara Ya Maji Yapongezwa

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, inayoongozwa na Mwenyekiti Jackson Kiswaga, imeridhishwa na ujenzi wa bwawa la maji katika Kijiji cha Kizengi, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Kiswaga ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo na mabwawa mengine nchini, huku akisisitiza kasi iongezwe ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama haraka.

Bwawa hilo, linalojengwa kwa fedha za ndani, lina gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 4 na litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 5.1 za maji kwa mwaka, likinufaisha zaidi ya wananchi 90,000. Hadi sasa, mradi huo umekamilika kwa asilimia 60.

Kamati pia imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa seti tano za mitambo ya uchimbaji mabwawa ili kusaidia wananchi. Aidha, wamepongeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, na wataalam wa sekta hiyo kwa jitihada zao katika kusambaza huduma ya maji safi nchini.