Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, wamehimizwa kuhakikisha wanaratibu kwa umakini taarifa za utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita na kuzisemea kwa wananchi ili wawe na uelewa wa kina kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo, kilichofanyika leo, Machi 14, 2025, katika Ukumbi wa Ngome, jijini Dodoma.
Waziri Lukuvi amesisitiza kuwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wana majukumu makubwa, hivyo wanapaswa kuwa mfano wa uwajibikaji katika utekelezaji wa kazi za Serikali na usimamizi wa shughuli zake, ili waweze kuratibu na kuwasilisha taarifa za mafanikio kwa wananchi.
"Tunalo jukumu la kuwaeleza wananchi kazi zilizotekelezwa na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi. Hili ni jukumu la msingi la uratibu, kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo yanayofanyika," amesema Waziri Lukuvi.
Aliongeza kuwa ili uratibu wa taarifa za Serikali uwe wa mafanikio, ni muhimu kuhakikisha kuwa majukumu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu yanasimamiwa vyema, kwani kufanya hivyo kutaiwezesha ofisi hiyo kusimamia ipasavyo taasisi na idara nyingine zilizo chini yake.
Aidha, Waziri Lukuvi alisisitiza kuwa Waziri Mkuu ana imani kubwa na watendaji wa ofisi yake, akiwataka waendelee kutekeleza jukumu la kuratibu shughuli zote za Serikali kwa ufanisi.
"Nikupongeze Katibu Mkuu, Dk. Yonazi, kwa usimamizi mzuri pamoja na timu yako ya menejimenti. Endeleeni kushirikiana katika kutekeleza majukumu yenu. Pia nawapongeza Wakuu wa Idara na Vitengo kwa kazi nzuri mnayofanya," amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, alimshukuru Waziri wa Nchi pamoja na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo kwa miongozo mizuri wanayotoa, akisisitiza kuwa hiyo imewezesha utendaji bora wa majukumu yao ya kila siku.
"Viongozi wetu wakuu wanafahamu kazi kubwa tunayoifanya. Kupitia nyie, tunawaomba mfikishe salamu zetu za shukrani kwao," amesema Dk. Yonazi.
Naye Msaidizi wa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE), Mkoa wa Dodoma, Maisha Mbilla, aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuhakikisha watumishi wake wanafanya kazi katika mazingira mazuri na wanapata stahiki zao ipasavyo.
"Hii inatufariji na kututia moyo. Sisi kama Chama cha Wafanyakazi tunao wajibu wa kuzungumza na watumishi ili waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma," amehimiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED