Kilogramu 980 taka za plastiki zakusanywa siku moja fukwe Kawe

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:13 PM Mar 17 2025
Kilogramu 980 taka za plastiki zakusanywa siku moja fukwe Kawe
Picha: Grace Mwakalinga
Kilogramu 980 taka za plastiki zakusanywa siku moja fukwe Kawe

KILOGRAMU 980 za taka za plastiki zimekusanywa katika ufukwe wa Kawe, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam katika kampeni ya usafi wa mazingira iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Taasisi ya Simply Green kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira, wamefanya ukusanyaji huo, huku wakiibua changamoto kubwa ya uchafuzi wa fukwe unaotokana na utupaji holela wa taka kwenye mito, mitaa na baharini.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Adriano Gesa, amesema licha ya juhudi za kufanya usafi, uchafu wa plastiki unaendelea kuwa tatizo kubwa, linalohitaji suluhisho la kudumu kupitia elimu na usimamizi mzuri wa taka.

“Tumefanya usafi katika eneo la mita 300 na tumekusanya kilogramu 980 za taka za plastiki, hili ni tatizo kubwa linalohitaji nguvu zaidi kukabiliana nalo, amesema Gesa.

Kilogramu 980 taka za plastiki zakusanywa siku moja fukwe Kawe
Amesisitiza kuwa pamoja na usafi wa fukwe, elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya taka za plastiki ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.

“Nawahamasisha wadau wa mazingira, kuendelea kutoa elimu kuhusu utunzaji wa fukwe, pia ni muhimu jamii kujenga utamaduni wa kutenganisha taka za majumbani ili kupunguza wingi wa taka za plastiki zinazotupwa kiholela,” ameongeza.

Gesa ametoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa za plastiki kuweka utaratibu maalum wa kukusanya na kudhibiti taka zao, ili zisilete madhara kwa afya ya binadamu na viumbe hai.

Kilogramu 980 taka za plastiki zakusanywa siku moja fukwe Kawe
Ofisa  Afya na Mazingira wa Kata ya Kawe, Joachim Kilawe, amebainisha kuwa usimamizi duni wa taka unaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, hasa yale yanayotokana na maji machafu.

“Taka za plastiki na uchafuzi wa mazingira vina Ongeza hatari ya magonjwa kama kipindupindu na kuhara, ni jukumu letu sote kuhakikisha tunadhibiti taka, ili kulinda afya ya jamii,” amesema Kilawe.

Amewahimiza wakazi wa Kawe kushiriki kikamilifu katika kutunza mazingira kwa kuhakikisha taka zinatupwa kwenye maeneo husika na kuchakata taka zinazoweza kutumika tena.