MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa, Michezo, Gerson Msigwa, amesema mchakato wa barabara ya haraka ya kulipia kati ya Kibaha hadi Chalinze haujakwama kama inavyozungumzwa na baadhi ya watu bali taratibu za utekezaji wake zinaendelea na upo katika hatua nzuri ya ununuzi.
Msigwa amesema majadiliano kati ya Wakala wa Barabara Tanzania-TANROADS na mbia yanaendelea ili kupata mradi unaoendana na thamani ya fedha na himilivu kwa serikali na watumiaji.
"Katika mwaka wa fedha 2022/23, serikali iliridhia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya haraka ya kulipia kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro (km 163.8). Maana baadhi walishaanza kusema mpango umefeli, nataka niwaambie mpango haujafeli, serikali inafanya maandalizi ili utekelezaji wake usije kuleta changamoto nyingi baadaye,” alisema Msigwa.
Alisema barabara hiyo ya kilometa 78.9 ambayo itakuwa ya kulipiwa, itatekelezwa kwa ubia kati ya sSekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Akizungumza juzi Kibaha mkoani Pwani baada ya kutembelea Kongani ya viwanda ya Sino-Tan iliyopo eneo la Kwala, Msigwa alisema, utekelezaji huo unafanyika baada ya serikali kufanya marekebisho katika sheria ya PPP sura namba 103.
Alisema utekelezaji huo ni pamoja pia na kanuni zake za mwaka 2020 na marekebisho ya mwaka 2023 yanayotaka kushirikisha sekta binafsi katika miradi ya maendeleo ya kimkakati.
Alisema lengo la serikali kushirikisha sekta binafsi ni kutanua wigo wa upatikanaji fedha.
"Tumefanya hivi kutokana na ukuaji wa mahitaji ya miundombinu ya barabara nchini, serikali imeamua kutumia njia ya ubia kwa kushirikisha sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi hii," alisema Msigwa.
Alisema utekelezaji wa mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili.
Msigwa alisema awamu nyingine ya utekelezaji wa mradi ni ule wa Chalinze-Morogoro, barabara ambayo alisema itakuwa na kilometa 84.9 na kwamba utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho za maandalizi.
Aidha, amesema upembuzi yakinifu umekwisha kamilika na tangazo kwa ajili ya manunuzi ya kupata wabia linatarajiwa kutolewa mwezi Mei, mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED