Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa ameagiza kuwa ifikapo Mei 12, mwaka huu saa sita usiku, ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini uwe umekamilika na minara yote 758 iwe imewashwa, ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano.
Waziri Silaa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini katika kijiji cha Kidete, Kata ya Chanzuru, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
“Rais Samia ametenga kiasi cha fedha Sh. bilioni 126 kwa ajili ya ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, ambapo kukamilika kwake kutapunguza changamoto ya mawasiliano nchini,” amesema Waziri Silaa.
Ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao milioni 8.5 waishio vijijini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED