Wanafunzi waiomba serikali kutenga fedha mafunzo kwa vitendo

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:49 PM Mar 15 2025
Wanafunzi wa Kilakala Sekondari wakiwa katika mafunzo kwa vitendo.
PICHA: SHABAN NJIA
Wanafunzi wa Kilakala Sekondari wakiwa katika mafunzo kwa vitendo.

WANAFUNZI 123 wa shule ya Sekondari ya Kilakala iliyopo mkoani Morogoro, wameiomba serikali kupitia wizara ya elimu kutenga fedha kwa ajili ya wanafunzi kwenda kujifunza kwa vitendo badala ya kuishia katika mafunzo ya nadharia darasani.

Hayo wameyabainisha leo wakati wa ziara yao ya kimasomo, kwenye mgodi wa Barrick Buzwagi uliopo kata ya Mwendakulima Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga na kuishauri serikali kuanza na kidato cha nne mpaka sita ambao ndio wako kwenye madarasa ya mitihani.

 Mmoja wa wanafunzi hao Consolata Ally wa kidato cha sita HGL, alisema wanafunzi wengi wanatamani kujifunza kwa vitendo lakini kutokana na uwezo mdogo wa wazazi na shule, wanabaki kukariri kwenye vitabu bila uelewa wa kutosha hali inayochangia wengi wao kufeli mitihani ya mwisho na kushindwa kujiajiri.

 Alisema endapo wanafunzi nchini watapewa fursa hiyo, Taifa litazalisha wasomi wengi wenye uelewa wa kutosha juu ya mambo wanayoyasoma ambayo mara nyingi wanayakuta kwenye uhalisia wa maisha baada ya kuhitimu masomo yao.

 “Sisi kama Kilakala tumepata fursa hii natumaini kwamba kuna wanafunzi wengi wangetamani kujifunza kwa vitendo ila hawana uwezo, serikali itenge fedha itakayotoa hizi fursa kwa wanafunzi na kutrngeneze wataalamu wenye ufahamu na kile wanachokisomea badala ya kuishia kukariri kwenye makaratasi tu” Alisema Consolata

 Mwingine Rebeca Masondowe wa kidato cha sita alisema, amejifunza kuhusu utunzaji wa mazingira na umuhimu wake kutokana na Barrick Buzwagi kusitiza shughuli za uzalishaji na sasa wanaendelea na urejeshaji wa mazingira katika hali ya kawaida sambamba na kulifanya eneo hilo kuwa la faida kwa jamii ya eneo husika.

 Mwalimu wa Sekondari hiyo, Grace Moshi, alisema kuna tofauti kati ya mwanafunzi aliyepata fursa ya kusoma kwa vitendo na ambaye amesoma tu darasani, kwani anakuwa na uelewa zaidi ya ambaye ameishia kwenye kitabu, haswa wanapoingia kwenye mitihani.

 “Mtoto ambaye yupo tu darasani, anajaza vitu kichwani anasubiri swali lije aliweke pale, anasoma anajaza vitu kichwani ambavyo hana uhakika navyo, lakini huyu aliyekuja kwenye 'field' (mafunzo kwa vitendo) hata swali litokee la namna gani yuko sawa kulijibu na atalijibu vizuri sana” alisema Mwalimu Grace 

 Awali Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Mgodini hapo, Stanley Joseph alisema wameendelea kuwapokea wanafunzi kwa nyakati tofauti ili kurithisha umuhimu wa uchimbaji salama wa madini unaoacha alama kwenye jamii ya eneo husika kupitia sekta ya afya, maji, elimu, kilimo na barabara.

 “Tumesitisha uchimbaji wa madini mwaka 2019 na uchakataji mwaka 2021, lakini ufungaji wa mgodi utakwenda mpaka 2027 kwa maana ya kurejesha mazingira katika hali ya kawaida kwa kupanda miti. Eneo hili sasa ni ukanda maalum wa kiuchumi na halmashauri itaendelea kunufaika kwa kupata mapato kupitia wawekezaji wapya" Alisema Joseph

 Aliongeza “Tunataka wanafunzi mfahamu umuhimu wa uchimbaji wa madini kwa sababu karibu kila kitu kinachotumika kwenye mazingira yetu ya kila siku kinatokana na madini, magari, saa tunazovaa na vitu vingine vingi, lakini kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.