Afrika Kusini yasikitishwa uamuzi wa Marekani kumfukuza balozi wake

By Enock Charles , Nipashe
Published at 01:08 PM Mar 15 2025
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa
PICHA: MTANDAO
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

Utawala wa Afrika Kusini umesema uamuzi wa Marekani wa kumfukuza balozi wake ni wa kusikitisha.

Hii inafuatia taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, akitangaza kuwa balozi wa Afrika Kusini ni mtu asiyekaribishwa na kumshutumu kwa ubaguzi.

Afrika Kusini imehimiza kuwa pande zote zinazohusika katika kudumisha staha ya kidiplomasia wakati wanashughulikia suala hilo.

Iliongeza kuwa bado imejitolea kuhakikisha uwepo wa uhusiano wenye tija na Marekani.

Hayo ndio yaliyojiri hivi karibuni katika mzozo wa kidiplomasia unaoendelea kutokota kati ya utawala mpya wa Marekani na Afrika Kusini.

Waziri Rubio alimkosoa Balozi wa Afrika Kusini nchini Marekani, Emrahim Rasool, kwenye mitandao ya kijamii, akiweka kiunganishi cha makala ambayo ilionesha maoni ya Balozi Rasool aliyotoa katika semina iliyofanyika mtandaoni Rasool aliripotiwa kushutumu utawala wa Trump kwa kuongoza harakati za kuamini kuwa kundi fulani ni bora kuliko wengine kote duniani.

Rais wa Marekani Donald Trump ameshutumu serikali ya Afrika Kusini kwa kuchukua ardhi kutoka kwa wakulima wazungu.

Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai hayo mara kwa mara. Wiki iliyopita Trump alitoa uraia kwa wakulima wa Afrika Kusini ambao wanataka kuondoka nchini humo.