Doyo wa NLD atangaza nia kuwania Urais

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 11:53 AM Mar 15 2025
Katibu  Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD) ,Doyo Hassan Doyo akitangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
PICHA: MTANDAO
Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD) ,Doyo Hassan Doyo akitangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

HATIMAYE kinyang’anyiro cha mbio za kutaka Urais kimepamba moto baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD) ,Doyo Hassan Doyo kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Doyo ametangaza kuingia katika kinyanganyiro hicho mbele ya waandishi wa habari mjini Morogoro baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kilichofanyika mjini hapa.

Ametaja vigezo na sifa ambazo alisema zinamruhusu kuwania nafasi hiyo ni pamoja na  umri usiopungua miaka 45 uliotamkwa ndani ya Katiba  ambao  tayari ameshavuka na pia anayo afya njema inayomuwezesha  kuhimili nafasi hiyo.

“ Mimi ni mwanachama wa NLD ,naweka wazi kuwa nitagombea nafasi ya urais kupitia Chama chetu,iwapo chama kitanipitisha kuwa mgombea na nitapambana mpaka kushinda uchaguzi huo” amesema Doyo.

Alifafanua  kilichomsukuma kuomba nafasi  hiyo ya urais inatokana na utafiti aliofanya na kubaini yapo  masuala ambayo hayajafanyiwa kazi ndani ya  nchi yetu.

Aliyataja ni pamoja na tatizo la ajira ,elimu , kilimo na ufugaji ,rasilimali za maji na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi, kupambana na rushwa kwa kiwango kikubwa kabisa.

Eneo jingine ni kujenga taifa la walipa kodi kwa kiwango kinachotahili, kuongeza nguvu katika sekta ya madini na kuongeza jitihada kwa watoto wa kike katika kupata elimu na teknolojia .

Jingine ni kuimarisha Muungano pamoja na kuimarisha sekta binafsi ili kukuza na kuongeza tija na ufanisi wa utendaji wa shughuli za kiserikali na kijamii.

Amesema chama hicho  kimepanga kuwafikia watanzania maeneo yote huku akiahidi  kufanya kampeni za kiustarabu za kunadi sera na  vipaumbele vyao ili wapigiwe kura .

“ Chama chetu  kinakusudia kuzindua sera  na ilani ya uchaguzi  Aprili mwaka huu jijini Dar es Salaam na tunakaribisha vyama vingine vyote na wananchi  kuja kusikiliza  “ alisema Doyo.

Akizungumzia kuhusu nafasi zingine katika uchaguzi huo ,Doyo alisema pia dhamira ya chama hicho ni kusimamisha wagombea wa Ubunge katika majimbo yote nchini pamoja na  madiwani wapatao 2,500 hadi 3,000 kulingana na jiografia ilivyo.

Nacho Chama cha DP(Democratic Party) kimesema kitashiriki kikamilifu uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kimeshatoa kalenda na kwamba mkutano mkuu wa chama utafanyika Juni mwaka huu mkoani Morogoro.