Putin ataka wanajeshi wa Ukraine walionasa katika eneo la Urusi wajisalimishe

By Enock Charles , Nipashe
Published at 01:11 PM Mar 15 2025
Rais wa Urusi Vladimir Putin
PICHA: MTANDAO
Rais wa Urusi Vladimir Putin

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewataka wanajeshi wa Ukraine walionasa katika eneo la Urusi la Kursk wajisalimishe huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akimtuhumu kiongozi huyo wa Urusi kwa kujaribu kuvuruga mpango wa usitishaji mapigano.


Rais wa Marekani Donald Trump amemhimiza Putin ayaokoe maisha ya vikosi vya Ukraine huku akisema mjumbe wake maalumu amefanya mazungumzo yenye tija na kiongozi wa Urusi kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano kwa kipindi cha siku 30.

Urusi imefanya mashambulizi ya haraka katika eneo la mpaka wa magharibi la Kursk katika wiki iliyopita, ikilikomboa eneo kubwa la ardhi iliyokuwa imetekwa na kudhibitiwa na Ukraine katika uvamizi wa kushangaza Agosti mwaka uliopita.

Kushindwa mjini Kursk kutakuwa pigo kubwa kwa mipango ya Ukraine kutumia udhibiti wake katika eneo hilo kama karata kwenye mazungumzo ya kutafuta amani kufuatia vita vilivyodumu miaka mitatu.

"Tunaunga mkono wito wa rais Trump," Putin alisema katika matamshi yake kwenye runinga ya Urusi. "Kama wataweza silaha zao chini na kujisalimisha, watahakikishiwa maisha yao na kufanyiwa vitendo vya heshima," Putin alisema.

Rais Trump alisema maalfu ya vikosi va Ukraine wamezungukwa kabisa na jeshi la Urusi na wako katika hali mbaya na ya hatari.


CHANZO: DW