Kamati ya Bunge yaridhiswa na uwekezaji PSSSF Sam Nujoma Complex

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:16 PM Mar 15 2025
Kamati ya Bunge yaridhiswa na uwekezaji PSSSF Sam Nujoma Complex.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamati ya Bunge yaridhiswa na uwekezaji PSSSF Sam Nujoma Complex.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuweza kuvutia wapangaji wakubwa katika uwekezaji wake katika jengo la kitegauchumi la PSSSF Sam Nujoma Complex lililopo jijini Dar es Salaam.

“Mafanikio ya uwekezaji huu wa PSSSF ni matokeo ya maono ya Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kunakuwepo na uwekezaji wenye tija. Pia nimefarijika kusikia kuwa mmeweza kuvutia wateja wakubwa kama taasisi mbalimbali za Serikali, Umoja wa Mataifa na Honora Tanzania (Tigo/Yas)” amesemaFatma Taufiq Mwenyekiti wa Kamati hiyo.


Kamati hiyo ipo katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya uwekezaji iliyo chini ya taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Festo Fute amesema, “Tumepokea mapendekezo yote, tunahakikisha tutayafanyia kazi kwa lengo la kuwa na uwekezaji wenye tija ambao pia utavutia wateja wapya.”


Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru amesema hadi sasa jengo hilo lina wapangaji kwa asilimia 70 na alihakikisha wataendelea kutoa huduma bora ili wateja waliopo wabaki na kuweza kuvutia wateja wapya.

Jengo PSSSF Commercial Complex ndilo jengo refu zaidi hapa Tanzania na ni moja kati ya majengo matatu marefu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Lina jumla ya ghorofa 35 na urefu wa mita 156.65. Jengo hili limeweka nakshi kwenye mandhari ya Jiji la Dar es Salaam na hii inadhihirishwa na muonekano wake kutokea pande zote za Jiji kutokea vilima vya Goba hadi Kigamboni, vilima vya Pugu hadi Kisiwa cha Mbudya.