Wajenga barabara kumuenzi Hayati Mengi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:52 PM Mar 16 2025
Wajenga barabara kumuenzi Hayati Mengi
Picha: Mpigapicha Wetu
Wajenga barabara kumuenzi Hayati Mengi

WANANCHI wa Kata ya Kibosho Kati, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamemuenzi kwa vitendo aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, kwa kupanua njia mbili za waenda kwa miguu, kuwa barabara zinazoziunganisha vijiji vitatu vya kata hiyo.

Kazi hiyo imetekelezwa na taasisi ya maendeleo ya kunusuru changamoto za wananchi wa kata hiyo (NAVIKA) kwa kukodisha katapila, kwa michango ya wanachama kwa zaidi ya Sh. milioni nne lakini thamani ya kazi itakayofanyika ni Sh. milioni 35. 

Wajenga barabara kumuenzi Hayati Mengi
Mwenyekiti wa NAVIKA, Paul Mushi, amesema wanachama wamejichanga fedha kutekeleza falsafa ya kitabu cha Dk. Mengi cha "I can, I Must, I will"  kwa kujiamini kuwa wanaweza badala ya kuisubiri serikali kuwafanyia. 

Aidha, amesema barabara zilizounganishwa ni ile ya Uchau, Kirima na Singa ambazo awali hazikuungana kutokana na kukososa vivuko vya kudumu.

WhatsApp Image 2025-03-16 at 16.48.39 (1).jpeg 843.08 KB
Mushi amewataka wananchi wa kata hiyo na Watanzania kwa jumla, kutumia nguvu na uwezo walionao kujiletea maendeleo kama alivyofanya Dk. Mengi na kuiwezesha jamii ya watanzania.

Diwani wa Kata Kibosho Kati, Bahati Mamboma, amesema kabla ya hatua wananchi wa vijiji hivyo vya Uchau, Kirima na Singa walikuwa wanatembea umbali wa zaidi ya kilomita nne hadi nane, kutokana na kukosekana kwa huduma za kijamii, hasa wanafunzi kwenda shule. 

Aidha, ameiomba serikali ijenge madaraja katika mito ya Uchau na Karanga na kuondoa vivuko vilivyopo sasa katika mito hiyo.

“Tunawashukuru Wakala wa Barabara Vijiji (TARURA), kwa kutusaidia utaalam kwa kuipima barabara hiyo, ili kupata viwango vinavyotakiwa,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kirima Juu, Duncan Mushi, amesema kupanuliwa kwa barabara hiyo ni ukombozi kwa wananchi ambao baadhi yao walipoteza maisha hasa wakati wa mvua.