Ahukumiwa kunyongwa kwa usafirishaji dawa za kulevya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:29 PM Mar 16 2025
Ahukumiwa kunyongwa kwa usafirishaji dawa za kulevya
Picha: Mtandao
Ahukumiwa kunyongwa kwa usafirishaji dawa za kulevya

MWANAMKE wa Kikenya, amekamatwa kwa usafirishaji wa dawa za kulevya huko Vietnam. Imepangwa kunyongwa kesho.

Vietnam ina sheria kali zaidi duniani kuhusu dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na adhabu ya kifo kwa yeyote anayekamatwa akisafirisha zaidi ya gramu 600 za heroini au kokeini.

Margaret Nduta Macharia, raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 37, anatarajiwa kunyongwa nchini Vietnam kesho, Jumatatu, Machi 17, 2025, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la usafirishaji wa dawa za kulevya.

Julai 2023, mamlaka za Vietnam zilimkamata Macharia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tân Sơn Nhất jijini Ho Chi Minh, baada ya kubaini zaidi ya kilo mbili za kokeini zilizofichwa ndani ya mzigo wake. Kabla ya kukamatwa Vietnam, alikuwa amesafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole nchini Ethiopia na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad nchini Qatar, bila kugundulika.

Wakati wa kesi yake, BMacharia alidai kuwa mwanamume Mkenya anayejulikana tu kama John alimwajiri kusafirisha mzigo huo kwa mwanamke mmoja nchini Laos, akilipwa dola 1,300 za Kimarekani huku gharama zake za usafiri zikigharamiwa. 

Alisisitiza kuwa hakujua yaliyomo kwenye mzigo huo. Hata hivyo, mahakama ilimkuta na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya mnamo Machi 6, 2025 na kumhukumu adhabu ya kifo.