KILA inapofika saa 12 jioni waumini waliofunga Kwaresma kwa wakristo na Ramadhani kwa waislamu hukusanyika kwa ajili ya futari. Hii ni hatua muhimu ya kutimiza ibada ya mfungo.
Wapo ambao hukaribisha ndugu, jamaa na marafiki kwa ajili ya futari kwenye eneo la nyumba, hotelini au kwingine kwa ajili ya kutimiza lengo la ibada hiyo, ambao hushiriki chakula na vinywaji kilichoandaliwa na muhusika.
Katika kipindi hiki hiki wapo wanaogeuza fursa ya kujipatia fedha au ushawishi wa nafasi au kura kutoka kwa wanaofanya ibada.
Wafanyabiashara wa mazao na bidhaa wanapandisha bei, wauzaji wa chakula wanapandisha bei maradufu na wanaotafuta ushawisi au kura wanawalisha waliofunga na kuwapa zawadi.
Nianze na wanaofuturusha, Imani ya dini ya Kiislam ina nguzo tano; ya kwanza ni Shahada yaani ungamo la imani ambalo hujumuisha kutamla kauli mbili: Hakuna mungu ila Allahna Muhammad Mtume wake.
Ya pili ni Salat; ni sala inayofuata utaratibu maalum mara tano kila siku; ya tatu ni Zakat inayomuelekeza muislam kuwangalia waislamu wenzake kwa hali na mali, na kushughulikia mahitaji yao ya maisha kwa kutoa fungu la mali yake.
Ya nne ni Funga au Saumu; yaani wakati wa mwezi wa Ramadhani kila mwislamu anapaswa kufunga chakula na kinywaji chote kuanzia asubuhi hadi jioni, ambapo watoto na wagonjwa hawapaswi kutekeleza wajibu huu.
Waislamu wanaona maana ya ibada hii kumkurubisha Mwislamu na Mola wake na kumfanya amche na kumuogopa zaidi, kwa kuwa saumu humsaidia Mwislamu kufahamu shida na taabu ambazo wale wasiokuwa na uwezo wanazipata wakiwa na njaa na hawana cha kukila, na kwa hivyo, huingiwa na huruma na kuwa na moyo wa kutaka kuwasaidia na kuwaondoshea shida hizo.
Na ya tano ni Hajj; Kila Mwislamu mwenye uwezo anatakiwa kwenda hijja Maka mara moja katika maisha yake wakati wa mwezi Dhul-Hija.
Zamani, ilikuwa watu kadhaa wa nyumba za jirani wanaandaa futari kwa mtu mmoja kwa maana kila mmoja anapeleka alichonacho kisha vinapikwa, alafu muda wa futari ukifika wanakula kwa pamoja.
Wakristo ni wakati wa siku 40 za Kwaresma kwa ajili ya toba, kufunga, kusali, kutafakari na matendo ya huruma, na katika kufunga huko wapo wanaofunga chakula kwa maana hawali chochote kuanzia asubuhi hadi saa 12 jioni, na kuna wanaokula na kufunga baadhi ya matendo.
Kila muumini huelekezwa kile anachojinyima (chakula) akipeleke kwa wenye mahitaji ambao ni maskini, yatima na wagonjwa ambacho ni sehemu ya matendo ya huruma kwa wanadamu wengine.
Kila unapoanza mfungo kilio kikubwa ni kupaa kwa bei ya mazao na bidhaa zinazotumika kuandaa futari hali inayowanufaisha wafanyabiashara ambao ndani yake kuna watu wa dini zilizopo kwenye mfungo.
Kwasasa unapotembea maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na kwenye mitandao ya kijamii unakutana na matangazo ya mahali kunauzwa futari, ambazo bei zake huanzia Sh. 10,000 kwa bufee (vyakula mchanganyiko) hadi Sh. 100,000, huku kikombe cha uji wa muhogo wenye viungo ukiuzwa kati ya Sh, 500 hadi 2,000.
Kilichoshangaza zaidi ni fasheni ya kufuturisha ambayo taasisi binafsi na mamlaka nyingine za serikali hushindana kufuturusha wadau wao kwa gharama kubwa, wenye majina (mastaa) na uwezo mkubwa kiuchumi hufuturushwa.
Imegeuka kuwa eneo la ‘show off’ kupata picha za kusambaza kwenye mitandao ya kijamii kujinadi kwa wateja na wadau kuliko matendo ya ibada na kuwasaidia wahitaji kupitia matendo ya huruma kama ambavyo dini zote zimeelekeza.
Wale wenye kumezaa mate nafasi mbalimbali za uongozi sasa wamepata njia ya kupitia wanafuturusha wajumbe na wapiga kura, kisha baada ya futari wanaondoka na vifurushi vya fitari waendako.
Ukiangalia yote haya hayafanyiki kwa lengo la ibada bali kunyonyesha kwa watu, kujitambulisha uwezo wa kifedha na kuwaonyesha makazi yao,biashara zao,na kuwafikia wajumbe, wapigakura na wafanya maamuzi kwenye ngazi mbalimbali kwa ajili ya kujipatia manufaa au upendeleo utakaendelea kuwaumiza maskini ambaye imani za dini zimeelekeza asaidiwe.
Sheikh Said Bafana katika moja ya video anaeleza kuwafuturisha watu wenye uwezo sio vibaya kwamba kuwaita rafiki nyumbani au hotelini na kufuturu pamoja kama njia ya kuunganisha undugu.
“Lakini kwa sasa imekuwa fasheni kwamba taasisi kubwa, benki kubwa wanafanya futari katika hoteli kubwa za gharama na watu wanaoitwa ni wadau na wateja kwa malengo ya kibiashara na si kumsaidia mtu asiye na uwezo,”anasema na kuongeza:
“Wapo ndugu zetu wengi wasio na uwezo vijijini wanaohitaji kupata futari au kubadili mlo wa siku lakini hawawezi, wale wanaoitwa na wakubwa (taasisi) wanaishia kugusa hawali chote mwishowe kinaishia kutupwa au wanaondoka na vifurushi. Hii ni kinyume na agizo la Mwenyezi Mungu.”
Ni muhimu jamii tukajikosoa kwamba kinachofanyika kinaendana na maelekezo ya imani tunazoamini au tunatumia imani kufanya yasiyostahiki, kama tumefikia hatua hiyo tumefika kubaya ambako tunahitaji kujisahihisha kama wanajamii.
Swali la kujiuliza tunafuturisha kwa ajili ya ibada au ‘show off’, rushwa? Mimi na wewe tujijibu.
Nawatakia Kwaresma na Ramadhani njema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED