Kamati ya PAC yaipongeza REA usambazaji umeme Singida vijijini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:13 PM Mar 15 2025
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Joseph Kakunda akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani Singida.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Joseph Kakunda akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani Singida.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Kaimu Mwenyekiti wake, Joseph Kakunda leo imetembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini mkoani Singida kupitia miradi ya awali kama vile REA Awamu ya Kwanza (REA I), REA Awamu ya Pili (REA II), REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza (REA III Round I), na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II); ambapo vijiji vyote 441 vya mkoa huo vimefikiwa na umeme huku vitongoji 1,052 vimefikiwa na huduma ya umeme kati ya vitongoji 2,289 vya mkoa wa Singida, sawa na asilimia 45.96 ya vitongoji vyote.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Joseph Kakunda ameipongeza Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Serikali kwa ujumla kwa kubuni, kuanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya kusambaza nishati ya umeme kwa wananchi wa mkoa wa Singida na kuongeza kuwa umeme ni fursa ya kuboresha maisha ya watu vijijini kama utatumika ipasavyo.

1


“Tumefurahishwa na tuliyoyaona hapa katika kijiji cha Kitopeni; Aghondi na kwenye zahanati ya kijiji cha Mabondeni. Tunaishukuru Serikali kupitia REA kwa udhibitisho wa uwepo wa umeme. Tunatoa wito kwa Wananchi, kasi ya kujiunganisha na huduma ya umeme, iongezeke; wekeni mpango ili kuhakikisha umeme unawasaidia kujiletea maendeleo yenu.” amesema, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Kakunda.
2

Katika taarifa yake mbele ya Kamati ya PAC; Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti Godfrey Chibulunje ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA; amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imetoa jumla ya shilingi bilioni 86.8 ili kuhakikisha miradi minne (4) inatekelezwa mkoani humo ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya umeme ili kuwapa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
3

“Wakala wa Nishati Vijijni (REA) unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na kuwasimamia kwa karibu makandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha wananchi.”amesema Godfrey Chibulunje.

Kamati ya PAC ipo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo inatarajia kufanya ziara hiyo katika mkoa wa Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam.