KUMBUKUMBU MIAKA 4 MAGUFULI; Askofu Niwemugizi asisitiza haki, uzalendo, kumuenzi JPM

By Daniel Limbe , Nipashe
Published at 01:20 PM Mar 17 2025
Janet Magufuli (katikati) pamoja viongozi wengine akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Janet Magufuli (katikati) pamoja viongozi wengine akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa

VIONGOZI wa umma wametakiwa kuongoza nchi kwa haki na kuimarisha upendo kwa jamii, ili kumuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Magufuli (JPM).

Magufuli, alifariki dunia Machi 17, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, ameyasema hayo wakati akiongoza ibada maalumu ya kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha Hayati Dk. Magufuli.

Amesema, wale waliochukizwa na kwa namna yoyote na utawala wake wamsamehe kwa kuwa ndiyo siri ya kuvuna baraka za Mwenyezi Mungu.

Waumini tofauti katika ibada
Kadhalika, amewataka viongozi hao, kuendelea kujifunza mema kutoka kwake kutokana na moyo wa uzalendo wa kuipenda nchi yake na kuhakikisha analinda kwa moyo wa dhati rasilimali za taifa.

"Dk. Magufuli alikuwa ni mwanadamu na kwa niaba yake mimi ninaomba kwa mabaya yoyote aliyotenda tumsamehe maana hayupo tena duniani na wasioweza kumsamehe mimi ninasema, hao siyo wakristo" amesema Askofu Niwemugizi.

Janet Magufuli, akiwasili kwenye ibada
Katika Ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Mariamzei Mlimani Rubambangwe Chato na kuongozwa na Askofu Niwemugizi, pia imetumika kutoa pole kwa mjane wa marehemu, Mama Janeth Magufuli pamoja na familia yote kwa ujumla kwa kuondokewa na mume, baba wa familia na kwamba wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa hatua hiyo kwa kuwa ni mpango wake kwa wanadamu.

Pamoja na mambo mengine, amesisitiza kila mmoja kuandika kitabu chake vizuri kingali bado hai, huku akisisitiza kuwa kila mwaka kanisa litaendelea kumwombea Hayati Magufuli, kutokana na mchango wake mkubwa kwa kanisa na taifa kwa ujumla.

Kadhalika amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutuma uwakilishi wake katika ushiriki wa maadhimisho ya ibada hiyo na kwamba Watanzania wanapaswa kuendelea kuishi kwa upendo na mshikamano.

"Tunayakumbuka maisha ya Hayati Dk. Magufuli, kwa mambo mengi aliyotenda enzi za uhai wake, maana alitambua na wakati wote alisisitiza maneno tumtangulize Mungu na tumrudie Mungu.

“Ndiyo maana tunamwombea yeye pamoja na viongozi walioko madarakani, kwa maana watu wanataka waishi kwa amani na utulivu," amesema Askofu Niwemugizi.

Katika ibada hiyo, viongozi mbalimbali wa chama na serikali wamehudhuria, akiwamo mwakilishi wa Rais Samia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, Makamu Mwenyekiti UVCCM Taifa, Rehema Sombi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Elias Kasendamila na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Luhumbi.