Wakati Serikali ilipoamua kuhamisha Stendi ya Mabasi ya Ubungo kwenda Mbezi Luis mwaka 2020, wengi waliutafsiri uamuzi huo kama kukata mshipa wa uhai wa kiuchumi wa eneo la Ubungo.
Hofu zilienea kwamba wajasiriamali, mama lishe, wauza magazeti na wasafiri wangeukosa mtandao wa kiuchumi uliojijenga kwa miongo kadhaa katika eneo hilo.
Lakini leo, Ijumaa Agosti 1,2025 historia imeandikwa upya, baada ya Ubungo kuzaliwa upya kwa sura kubwa na yenye mwelekeo wa kikanda na kimataifa kwa kuzinduliwa kwa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC).
Katika hali hiyo ya mabadiliko chanya, uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan unapaswa kupongezwa kwa weledi na maono ya kugeuza changamoto kuwa fursa za maendeleo ya kiuchumi na ajira kwa maelfu ya Watanzania.
Uhamishaji wa stendi ya Ubungo kwenda Mbezi Luis haukulenga kupunguza msongamano wa magari pekee, bali mpango wa kufungua sura mpya ya kibiashara inayoendana na mikakati ya maendeleo ya kisasa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26, Serikali imeweka kipaumbele katika kuendeleza miundombinu ya biashara, ikiwemo maeneo ya kimkakati ya biashara ya kikanda. EACLC ni matokeo ya utekelezaji wa mpango huo.
Lango jipya ya uchumi wa kikanda
EACLC ni zaidi ya soko au jengo linaloshuhudiwa. Ni muhimili wa kimkakati wa kibiashara unaolenga kuunganisha nchi za Afrika Mashariki kwa kuwezesha urahisi wa biashara, usambazaji wa bidhaa na huduma na matumizi ya teknolojia kuongeza tija.
Hii ni nguzo muhimu ya utekelezaji wa Ndoto ya Soko la Pamoja Afrika kupitia Itifaki ya Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA).
Manufaa ya moja kwa moja
Kwa mujibu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kituo hicho kimeanza kutoa zaidi ya 3,000 za moja kwa moja, huku zisizo za moja kwa moja zikitarajiwa kutolewa zaidi ya 10,000 ifikapo 2026.
Pamoja na ajira, EACLC kinakadiriwa kuongeza mapato ya Serikali kwa zaidi ya TZS bilioni 50 kwa mwaka, kupitia kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kodi ya mapato, ada za leseni na tozo za manispaa.
EACLC inatarajiwa kuwa kituo kikuu cha wafanyabiashara kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na hata nchi za SADC. Tayari zaidi ya wawekezaji 300 kutoka nje ya Tanzania wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye kituo hicho.
Kwa mujibu wa ripoti ya World Bank Logistics Performance Index (2023), gharama ya usafirishaji bidhaa Afrika Mashariki ni kati ya asilimia 18-22 ya thamani ya bidhaa, ikilinganishwa na asilimia nane barani Ulaya.
EACLC inatarajiwa kupunguza gharama hizo kwa asilimia tano hadi nane, kwa kuweka mifumo ya haraka na teknolojia ya kisasa ya usafirishaji.
Rais Dkt. Samia kiongozi wa maono ya kikanda
Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa EACLC, Rais Dk. Samia amesisitiza kuwa kituo hiki hakipingani na Soko la Kariakoo, bali kinapanua wigo wa fursa za kibiashara na kutoa nafasi ya kujifunza namna teknolojia inavyoweza kuongeza thamani ya bidhaa. Hili ni jambo la msingi katika zama za uchumi wa kidijitali.
Ni muhimu kuelewa kwamba ujenzi wa EACLC ni sehemu ya azma ya Rais Dkt. Samia ya kutengeneza Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji wa kikanda.
Ubungo katika sura mpya
Wengi walihofu kuwa Ubungo ingekufa kiuchumi baada ya kuondolewa stendi. Kinyume chake, EACLC imerejesha uhai wa eneo hilo kwa namna ya kisasa zaidi.
Asilimia 95 ya maduka kwenye kituo hicho yamekodishwa. Huduma za kibenki, bima, uagizaji bidhaa na huduma za kidijitali zimeanzishwa.
Miundombinu ya kisasa imesimikwa, ikiwa ni pamoja na barabara za ndani, mtandao wa intaneti ya kasi, maegesho ya malori na mfumo wa kamera za usalama.
Tunaposema mitano tena na 'Oktoba tunatiki' tunamaanisha na hatulengi uongozi tu, bali kuendelezwa kwa sera bora zenye maslahi kiuchumi chini ya Dk.Samia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED