Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya 32 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) ya mwaka 2025, yaliyoanza leo Agosti 1, 2025.
Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Omega Ngole, PSSSF inashiriki kwenye Maonesho yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma, Zanzibar, Kanda ya Magharibi Tabora na Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
" Wanachama wakiwemo wastaafu wetu watakaotembela kwenye mabanda yetu, watapewa mwongozo wa kujiunga na huduma za Mfuko kidijitali kwa kutumia simu janja, kuhuisha taarifa na kuhakiki taarifa zao, kupata ufafanuzi wa taarifa mbalimbali za Mafao.” Alifafanua Bw. Ngole
Aidha, Wanachama na wananachi wanakaribishwa ili wapate taarifa za fursa zitokanazo na miradi ya uwekezaji iliyofanywa na mfuko kwenye maeneo ya viwanda.
" Ukitembeela banda letu hapa Nzuguni Dodoma, utajionea matokeo ya uwekezaji huo kwa kununua bidhaa za Ngozi kama vile viatu, mikoba na mikanda kutoka kiwanda cha KLICL kilichoko Kilimanjaro ambacho mfuko umewekeza, pia wananchi wataweza kununua nyama safi yenye viwango vya kimataifa kutoka Machinjio ya Ranchi ya Nguru mkoani Morogoro.” alifafanua.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maonesho hayo ni: 'Kilimo ni Biashara: Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi'
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED