Simanzi nyumbani kwa mfanyabiashara aliyeuawa na kufukiwa porini

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 10:17 PM Aug 01 2025
Simanzi zatawala nyumbani kwa mfanyabiashara aliyegundulika kuuawa na kufukiwa porini Kilosa
Picha:Mpigapicha Wetu
Simanzi zatawala nyumbani kwa mfanyabiashara aliyegundulika kuuawa na kufukiwa porini Kilosa

Simanzi na majonzi vimetawala nyumbani kwa marehemu William Chitemo, mfanyabiashara wa ng’ombe kutoka Kijiji cha Mtumbatu, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, baada ya mwili wake kupatikana umefukiwa porini katika Kijiji cha Tame, Kata ya Mamboya.

Mtoto wa marehemu, Jackson Chitemo, amesema familia ilihangaika kumtafuta baba yao tangu alipopotea Julai 28, 2025, lakini haikutarajia kupata taarifa za kusikitisha kama hizo.

 Mke wa marehemu, Happyness Mjoe, amesema bado haamini kama mume wake hayupo tena kwani aliondoka kwa nia ya kutafuta Ng'ombe hadi walipopata taarifa za kukutwa kwa mwili wake ukiwa umefukiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema mwili wa marehemu William Chitemo, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45 hadi 50, ulikutwa umefukiwa baada ya taarifa za awali kuonyesha kuwa mara ya mwisho alionekana akitumia pikipiki aina ya Haujue yenye namba za usajili MC 221 DWW, akielekea kununua ng’ombe baada ya kuitwa na mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa uchunguzi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtumbatu, Bi Veronica Kalaita, amesema tukio hilo limeishtua jamii, na ametaka hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika ili iwe fundisho kwa wengine.

Tukio hilo limezua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo, huku wito ukitolewa kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kufichua uhalifu unaojitokeza katika jamii.