CHAUMA yaahidi makubwa Morogoro

By Christina Haule , Nipashe
Published at 01:03 PM Aug 02 2025
news
Picha Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa CHAUMMA Taifa Devotha Minja

CHAMA cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA kimewaomba wananchi kuwapa ridhaa wanachama wanaogombea kwenye nafasi za ubunge na udiwani nchini ili kutatua changamoto mbalimbali za kijamii zinazotatulika kwa kukuza uchumi wa watanzania.

Makamu Mwenyekiti wa CHAUMMA Taifa Devotha Minja amesema hayo leo wakati akizungmza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapo.

Anasema Morogoro imekuwa kama haina mwenyewe sababu barabara haziridhishi, watumishi wa umma hawana mishahara ya kueleweka na kuishia kukimbilia kuwa bodaboda baada ya kazi ili kukidhi mahitaji yao.

“Niwasisitize wakazi wa Morogoro kubadilika na kuacha akili za kukubali misaada isiyoeleweka ya kuzika bila kupata msaada wa kuuguza,” amesema.

Amesema wanamshukuru hayati Mwalimu Julius Nyerere kwasababu Morogoro hawalimi Tumbaku wala Pamba lakini wakaletewa viwanda na mtu mmoja akaja kuzika maendeleo hayo hivyo watakuja kubadilisha na kurejesha viwanda hivyo ambavyo vimeondolewa na mtu mmoja kwa maslahi yake binafsi.

Aidha, amevitaka vyama vya siasa vingine kuamua na kushirikiana na CHAUMA kuiondoa CCM iliyopo madarakani ambayo haitendi yaliyo sawa. Na umoja wao huo utasaidia kulinda kura zao ili zisiondoke.

Devotha amesema tayari amechukua fomu ya ubunge Kata Morogoro mjini ambapo wagombea udiwani katika Manispaa ya Morogoro kwenye Kata zote 29 wameshachukuaa fomu.

Akitoa salama za mwenyekiti wa chama hicho Hashm Rungwe, amesema sera ya Ubwabwa itaendelezwa na CHAUMA kwasababu ili taifa lipate maendeleo lazima lipate chakula.

Amesema kazi ya kwanza ya CHAUMMA ikiingia madarakani lazima Watanzania wapate chakula kwasababu kuna mashamba mengi ya kulima ambako kilimo kinaweza kumsaidia mtu chakula atauza na kupata fedha, huku taifa likipiga hatua kimaendeleo.

Amesema wakiingia madarakani watahakikisha wanatumia fedha za bandari, madini na kodi na kuhakikisha Watanzania wanapata chakula.