“Kituo cha Biashara Ubungo hakitaua K’koo”

By Restuta James , Nipashe
Published at 03:38 PM Aug 02 2025
news
Picha Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo Dar es Salaam.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Dar es Salaam, kuwa Kituo kipya cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC), hakitakuwa mshindani wao, bali kitalisaidia Taifa kufikia malengo mapana ya viwanda na biashara.

Amesema kitakuwa jukwaa la kimkakati kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa, kutengeneza ajira na kukuza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kimataifa.

Rais Samia aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua kituo hicho, kilichoko Manispaa ya Ubungo.

“Kuwapo kwa kituo hiki, si mshindani wa Soko la Kariakoo. Soko la Kariakoo limejenga jina muda mrefu, lakini bado linahitaji kusoma. Badala ya kuwa mshindani, (EACLC) kiwe mwalimu,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wa Kariakoo wanapaswa kukitumia kujifunza mbinu za kufanyabiashara kwa mifumo ya kiteknolojia, itakayowezesha ukuaji wa uchumi na mapato ya serikali.

Rais Samia alisema mradi huo ni mkakati wa kutatua changamoto za kibiashara na usafirishaji, zilizokuwa zinaikabili Tanzania pamoja na nchi jirani, huku ukiifanya nchi kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara.

“Masuala ya ukosefu wa miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara, gharama kubwa za uendeshaji wa biashara, yanakwenda kutatuliwa na miradi hii.

“Kupitia kituo hiki, wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, wataweza kufanikisha shughuli zao kwa urahisi zaidi, kwa kutumia mifumo ya kisasa. Kwa msingi huo, ninawapongeza wawekezaji kwa ujenzi wa kituo hiki ambacho kitakuza ushirikiano baina ya sekta za biashara za China na Tanzania,” alisema Rais Samia.

Alisema EACLC kitatumika pia kama eneo la kuhamasisha bidhaa za Tanzania kwenda kwenye masoko ya China na nchi nyingine. 

“Nimekutana na vijana wa Tanzania, wanaotumia rasilimali za Tanzania kama mkonge na mazao mengine ya kilimo, kutengeneza vifaa vya kuuzwa nje ya nchi,” alisema.

Alisema kwa kufanya hivyo, itachochea mauzo ya Tanzania nje ya nchi, kuongeza mapato ya serikali na ya Manipaa ya Ubungo, upatikanaji wa fedha za kigeni, pamoja na ajira kwa vijana wa Tanzania.

Alisema kituo hicho ni jukwaa la kuwaunganisha wazalishaji, wasafirishaji, wasambazaji, watumiaji na walaji, kutoka ndani na nje ya nchi, kitakachoongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kuifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza kwa wafanyabiashara.

Aidha, aliwahimiza vijana nchini kutumia fursa za ajira zinazotolewa badala ya kulaumu kwamba serikali haiwaoni.

“Tunaposema serikali tunatengeneza mazingira kwa vijana, haya ndiyo mazingira yenyewe. Sasa ni nyinyi kutumia fursa hizi. Kutumia kama mnavyoonyesha hapa, kutengeneza vitu tuwauzie nje. 

“Msitulaumu serikali hatuoni; kuona kwenyewe ndiyo hivi. Serikali haiwezi kuja kwa mmoja mmoja ikampa hivi, lakini tumetengeneza mazingira, myatumie,” alisema.

Rais Samia aliwataka wazalishaji nchini kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaoendana na hadhi ya jina la Tanzania.

“Zalisheni kwa viwango. Nisisitize kuzalisha kwa viwango sababu bidhaa yoyote itakayotoka na alama au maneno kwamba imezaliwa Tanzania lazima itoke na viwango kama jina letu lilivyo na viwango,” alisema.

Balozi wa China Nchini, Chen Mingjian, alipongeza uhusiano imara na wa kihistoria kati ya mataifa haya mawili, ulioasisiwa na waasisi wao, Mao Zedong na Mwalimu Julius Nyerere.

“China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Tanzania kwa miaka tisa mfululizo, na kiasi cha biashara kilizidi Dola za Marekani bilioni 8.88 mwaka 2024,” alibainisha balozi huyo.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, alisema kuzinduliwa kwa mradi huo, kuna dhihirisha dhamira ya Rais Samia ya kuifungua nchi.

Alisema ndani ya wiki moja, Rais Samia amezindua miradi minne mikubwa akianzia wilayani Namtumbo, alikozindua Kiwanda cha Kuchakata Madini ya Urani, Kongani ya Viwanda Kibaha, Bandari ya Kwala na kituo hicho cha biashara.

“Miradi yote ambayo umeifungua wiki hii, ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050 hususani nguzo ya kwanza inayozungumzia, kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani," alisema.

Aidha, alisema mwaka 2020, Jimbo la Ubungo lilikuwa na biashara 4,000, na sasa zimefikia 8,997, huku idadi ya maduka ikiongezeka kutoka 2,825 hadi 6,449.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, alisema uwekezaji katika mradi huo, umeingiza mtaji wa Sh. bilioni 282 na kutoa ajira zaidi ya 2,000 wakati wa ujenzi.

Alisema kwa sasa mradi huo utatengeneza ajira 65,000 zikiwamo moja kwa moja 15,000 na zisizo za moja kwa moja 50,000 pamoja na vizimba 2,060.

Mwenyekiti wa EACLC, Dk. Lisa Wang Xiangyun, alisema mbali ya kuzalisha ajira, kituo hicho kinatarajiwa kusaidia zaidi ya biashara ndogo na za kati 500, na kupunguza gharama za biashara kikanda kwa asilimia 30.