WACHUMI nchini wameonyesha matumaini yao kwenye programu ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) katika kupaisha uchumi wa Tanzania, huku wakiihusisha katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamejiri baada ya siku chache kupita tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuongoza uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uliofanyika mkoani Dodoma.
Mchambuzi wa Masuala ya Kiuchumi na Kisiasa Mahimbo Denis, anasema baada ya kuisoma vizuri dira hiyo na kuielewa anaifungamanisha na nafasi ya Ubia katia ya Sekta ya Umma na Binafsi katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Anasema ni vyema kufahamu maana ya PPP na chimbuko lake katika nchi zinazoendelea hususan nchi zilizopo ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa ni moja wapo.
Anafafanua kuwa dhana ya ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ilipata chapuo mwanzoni mwa miaka ya 1990, hasa ikiwa ni sehemu ya Programu ya Marekebisho ya Miundo/Mifumo (SAPs).
Anasema tokea hapo matumizi yake yamekua yakiongezeka na kukua katika nchi mbalimbali huku nchi hizo zikiweka taratibu kama vile kutunga/kutengeneza sheria za makubaliano.
“Utekelezaji wa PPP umekua ukitofautiana kutoka nchi moja hadi nyingi huku na kimsingi dhana hii tokea kuanzishwa kwake miaka hiyo ya 1990s imekuja kupata kueleweka na kutumika vyema hasa kufikika miaka ya 2010s.
“Nchi kama Misri, Ghana, Morocco, Nigeria, na Africa Kusini zilikuwa ni miongoni mwa nchi za kwanza kutekeleza miradi mikubwa kwa njia ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,” anasema.
Anaongeza kuwa ili kuelewa vizuri Dira 2050 ni vyema kujua japo kwa ufupi kuhusu ili kupata uhusiano wa kimantiki na kithemanti wa dira hiyo.
Anasema katika kujiwekea mipango thabiti ya maendeleo, mwaka 2000 Tanzania ilizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ambayo ililenga kulijenga taifa kuwa nchi ya kipato cha kati. Maeneo ya kipaumbele yalikuwa ni kilimo cha kisasa, viwanda, miundombinu na teknolojia.
“Dira 2025 imeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, huku ikishuhudia ukuaji wa uchumi, na utawala, Tangu kuzinduliwa mwaka 2000, Tanzania ilidumisha kasi ya ukuaji endelevu wa Uchumi ambako pato halisi la taifa liliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa mwaka kati ya 2000 na 2024,” anasema.
Anasema mafanikio mengine yaliyopatikana ni: kuongezeka kwa wastani wa umri wa kuishi kutoka miaka 51, 2000 hadi miaka 68, 2024, kupungua kwa vifo vinavyotokana na uzazi kutoka 750 kwa kila vizazi hai 100,000 2000 hadi asilimia 79.9 vijijini na 94 mijini 2024.
Kwa ujumla, utekelezaji wa Dira 2025 umeimarisha msingi wa maendeleo ya watu, uchumi wa taifa na mwelekeo wa ustawi jumuishi unaozingatia maslahi ya Watanzania wote.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Tanzania haikufanikisha kikamilifu malengo yote ya Dira 2025. Ingawa nchi ilifikia hadhi ya Uchumi wa kipato cha kati ngazi ya chini na pato la mtu mmoja mmoja liliongezeka, haikufikia kuwa na lengo la wastani wa dola za Marekani 3,000 kwa mwaka.
Dira 2050 inalenga baada ya miaka 25 ijayo, Tanzania ije kuwa ni nchi ya mfano katika ustahimilivu, ubunifu ustawi na diplomasia barani Africa na duniani huku ikichochewa na rasilimali zake, miundombinu imara na nguvu kazi mahiri na yenye motisha.
Anasema Tanzania inategemewa kuwa nchi yenye kipato cha kati ngazi ya juu huku ikiwa na pato la taifa lenye thamani ya dola za kimarekeni trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja mmoja lenye thamani ya dola za kimarekani 7,000.
Anasema uchumi wake utakuwa shindani na mseto, unaotegemea viwanda huku ukichagizwa na nguvukazi yenye maarifa na ujuzi.
Pia anasema dira imeweka wazi kuwa ili kufanikisha adhma hiyo, yanahitajika mabadiliko ya haraka na ya kina, yakiwemo mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, kilimo chenye tija zaidi, umeme wa uhakika, na kuendeleza ujenzi mkubwa zaidi wa miundombinu ya kisasa.
Anasema dira 2025 inaeleza bayana kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi,
“Dira 2050 inalenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuiwezesha sekta hiyo kuwa imara na shirikishi ili kuendeleza uvumbuzi, ubunifu na ukuaji endelevu.
“Dira hii pia inalenga kufanya mabadiliko na mageuzi makubwa katika sekta binafsi huku ikitoa fursa sawa za kiuchumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” anasema.
Kwa kuzingatia mafanikio na uzoefu uliopatikana kutoka dira 2025, dira 2050 inalenga kuiwezesha Tanzania kutumia rasilimali zake kikamilifu ili kujiletea maendeleo na hivyo kuwa taifa lenye nguvu kiuchumi barani Afrika na kwingineko.
NAFSI YA PPPC
Anasema kama mchambuzi wa kisiasa na kiuchumi, anaiona taswira na dhamira ya dhati ya serikali kupitia PPPC kama ndicho chombo kinachoaminiwa na kukasimiwa jukumu kubwa la kuiwezesha serikali kufikia malengo yaliyomo kwenye dira 2050.
Anaeleza kuwa lengo la dira inayoisha muda wake (2025) ilikuwa ni kufikia wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kufikia dola za Marekani 3,000 na sasa lengo hilo limewekwa kuwa wastani wa Dola 7,000 kwa mwaka kufikia mwaka 2050.
Anasema malengo hayo ni makubwa lakini lipo tumaini la kuyafikia hayo yote kama PPPC itasimama kwenye zamu yake na kutekeleza kile kilichopo ndani ya uwezo wake.
Anasema tafiti na taarifa mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa sekta binafsi zimekua na mchango mkubwa sana katika kuleta maendeleo ya nchi na ikiwi ndiyo muajiri mkubwa duniani kote.
Katika kutekeleza miradi mbalimbali kwa njia ya ubia, kampuni kubwa duniani za ujenzi wa miundombinu kama vile China State Construction Engineering Corporation (CSCEC) na VINCI SA zinamchango mkubwa katika kuleta maendeleo, kwakua mbali na kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi pia zinaleta teknolojia na kupanua wigo wa ajira katika nchi husika.
“Leo hii, Kampuni kubwa duniani kama vile Nvidia, Apple,Tesla, Microsoft, na Amazon zimetoa mchango mkubwa katika mageuzi ya teknolojia na kuajiri maelfu. Apple ambayo ilianzishwa mwaka 1976 na Steve Jobs leo hii ina ukwasi usiopungua dola za kimarekani zaidi ya bilioni 600.
“Nchini Ufaransa kwamfano, kupitia dhana ya PPP imetekeleza mradi mkubwa wa kisasa wa usafiri ujulikanao kama ‘The Grand Paris Express’. Mradi huu umetekelezwa kwa ubia kati ya RATP Group ambayo ni kampuni ya serikali na VINCI Construction kampuni ilijenga/kutekeleza mraadi huo,” anasema.
Kadhalika anasema dira 2050 ni nyenzo hivyo ni muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku dhamira kuu ikiwa ni kujenga taifa lenye nguvukazi iliyoelimika, yenye ujuzi na maono, ambayo itafanikisha maendeleo endelevu.
Anaeleza kuwa nguvukazi hiyo itajengwa katika misingi ya ubunifu, ujasiriamali na uwajibikaji.
Makala hii imeandikwa na Mchambuzi wa Masuala ya Kiuchumi na Kisiasa Mahimbo Denis 0758414190
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED