Katibu Tawala Singida aitaka TVLA kuwafikia wafugaji vijijini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:48 PM Aug 02 2025
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma  Mganga akizungumza baada ya kutembelea banda la  Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA)
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga akizungumza baada ya kutembelea banda la Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA)

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma R. Mganga, ameitaka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuongeza juhudi za kuwafikia wafugaji wadogo waishio vijijini ili kutambua changamoto wanazokutana nazo hususan katika suala la uchanjaji wa mifugo.

Dk. Mganga ametoa wito huo leo Agosti 2, 2025, alipotembelea banda la TVLA lililopo ndani ya banda jumuishi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni jijini Dodoma.

“TVLA isiishie kuzalisha na kusambaza chanjo pekee, bali ifuatilie namna wataalamu wanavyofanya uchanjaji ili kuepusha madhara yasiyo ya lazima. Pia ni muhimu kufuatilia utekelezaji katika halmashauri zote na kufanya mikutano na wafugaji kwa kuwa wao ndiyo wadau wakuu,” 

“TVLA iendelee kujitangaza ili huduma inazozitoa ziwafikie wafugaji wengi zaidi na kusaidia kuinua uchumi wao, vilevile muwatembelea wafugaji kwani wengi wao hawana elimu ya kutosha kuhusiana na uchanjaji pamoja uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kwani Mifugo ikiwa na afya mazao yatokanoyo na Wanyama yatakuwa bora” alisema Dk. Mganga.

Dk. Mganga pia aliagiza wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Singida kukutana na Mtendaji Mkuu wa TVLA ili kujadili namna bora ya kushirikiana kufikisha huduma za chanjo kwa halmashauri zote za mkoa huo aidha, aliipongeza TVLA kwa juhudi za kuzalisha na kusambaza chanjo katika maeneo yote nchini na kutoa wito wa kuandaa mkakati utakaowawezesha wafugaji kununua chanjo kwa urahisi ili kulinda mifugo yao dhidi ya magonjwa.

Kwa upande wake, Dk. Isaac Mengele (PhD), Daktari wa Mifugo na Mtafiti Mwandamizi wa TVLA, alisema shirika hilo linashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma za maabara za veterinari, matumizi sahihi ya chanjo, tafiti za magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao magonjwa, pamoja na kutoa ushauri kwa wafugaji.

“TVLA imejipanga kuimarisha uzalishaji endelevu wa sekta ya mifugo, kuimarisha usalama wa chakula na kuchangia katika uchumi wa taifa kupitia huduma bora na nafuu za uchunguzi, utambuzi, uzalishaji wa bidhaa za veterinari, na utafiti wa magonjwa pamoja na wadudu waenezao magonjwa,” alisema Dk. Mengele.

Ziara hiyo iliambatana na viongozi wengine wakiwemo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, CPA Erick A. Nikahera; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Ndg. Mnyika Hassan; pamoja na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Kilimo.