DC Ludewa akoshwa ubunifu maandalizi Nane Nane

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 01:40 PM Aug 02 2025
news
Picha Julieth Mkireri
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, akikagua mabanda ya wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas ametembelea viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya kushiriki na kukagua mabanda ya halmashauri ya wilaya hiyo katika Maonyesho ya Kilimo ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza jana baada ya ukaguzi huo, Thomas amewapongeza wataalam na washiriki wa halmashauri hiyo kwa ubunifu, juhudi na maandalizi bora ya maonyesho hayo.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote kutembelea mabanda ya Halmashauri ya Ludewa ili kujifunza, kupata elimu ya kilimo bora, na kuona fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda.

“Tuna mambo mazuri sana hapa kutoka huduma za ugani hadi ubunifu wa viwanda vidogo. Wananchi mnakaribishwa kwa wingi kutembelea mabanda yetu ili kuona maendeleo ya Ludewa na kupata elimu ya kuboresha maisha yenu kupitia sekta ya kilimo na ufugaji,” amesema Thomas.

Maonyesho ya Nane Nane mwaka huu yanaendelea kuvutia wadau wengi wa kilimo kutoka mikoa mbalimbali, yakilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia, uongezaji thamani, na ubunifu kwa maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa 

1