Makosa ya jinai yapungua Zanzibar kwa asilimia 27.7

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 08:30 PM Aug 01 2025
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo

Jumla ya makosa 1,197 ya jinai yameripotiwa Zanzibar katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2025, yakionesha upungufu wa makosa 455 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana ambapo yalikuwa 1,652, sawa na asilimia 27.7.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo, amesema hayo leo Agosti 1, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar.

"Kupungua kwa makosa haya kunatokana na juhudi za pamoja za kutoa elimu kwa jamii kupitia ngazi za shehia, vyombo vya habari na kampeni mbalimbali za uhamasishaji ambazo zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya uhalifu," amesema Kamishna Kombo.

Makosa dhidi ya binadamu yapungua kwa asilimia 33.1

Amesema kati ya makosa 1,197 yaliyoripotiwa, makosa dhidi ya binadamu yalikuwa 409, yakionesha upungufu wa makosa 202 kutoka makosa 611 yaliyotokea mwaka jana – sawa na asilimia 33.1.

Makosa hayo ni pamoja na:

  • Mauaji – 26 kesi
  • Ubakaji – 338 kesi
  • Kulawiti – 42 kesi

Makosa mengine ya kijinai na usalama barabarani

Kamishna Kombo amesema aina nyingine za makosa yaliyosajiliwa ni pamoja na:

  • Kuwania mali – 755 kesi
  • Wizi kwa kuvunja – 283 kesi
  • Wizi wa mifugo – 195 kesi
  • Makosa ya barabarani – 28,740 kesi

Visababishi vya mauaji: wivu wa kimapenzi na ugomvi

Akifafanua kuhusu kesi za mauaji 26, Kamishna Kombo alisema asilimia 3 ya matukio hayo yamesababishwa na wivu wa kimapenzi, huku asilimia 6 yakitokana na ugomvi katika vilabu vya starehe. Sababu nyingine zinaendelea kuchunguzwa.

"Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu ya kupinga vitendo vya jinai na kuhakikisha Zanzibar inabaki kuwa mahali salama kwa wananchi na wageni," ameongeza Kombo.