Polisi: Ebitoke hajatekwa, yuko hospitali Mtwara

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:04 PM Aug 01 2025
 Anastanzia Exavery Mahatane maarufu kama Ebitoke.
Picha: Mtandao
Anastanzia Exavery Mahatane maarufu kama Ebitoke.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, limefanikiwa kumpata msanii wa vichekesho, Anastanzia Exavery Mahatane maarufu kama Ebitoke, baada ya kumkuta katika hali ya kuchanganyikiwa na kumpeleka Hospitali ya Mkoa wa Mtwara kwa matibabu.

Taarifa ya  Kamanda wa Polisi Mtwara Issa Suleiman iliyotolewa leo Agosti Mosi, 2025, imetaka ndugu wa msanii huyo kujitokeza ili kumsaidia.

Kupatikana kwa Ebitoke, kunafuatia msanii huyo kuchapisha taarifa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kwamba kuna watu wanataka kumuua.

Polisi wamesema baada ya taarifa hiyo, walianza uchunguzi na kumkuta katika Kata na Kijjiji cha Msanga Mkuu, mkoani humo.

Taarifa ya Polisi imesema kuwa uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo umebaini kwamba Ebitoke alifika mkoani Mtwara tangu Aprili mwaka huu 2025 na kufikia katika hoteli moja iliyopo Msanga Mkuu, na kuomba hifadhi kwa watu waliokuwa wanafahamiana kabla ya maisha yake kumuendea vibaya.

“Tarehe 31 Julai, 2025 saa 11:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara lilimkamata Anastanzia Mahatane huko katika fukwe za Msanga Mkuu akiwa katika hali inayoonekana kuwa amechanganyikiwa na wala hakuwa ametumbukizwa katika shimo wala kutekwa kama ambavyo alivyokuwa ameeleza katika mitandao hiyo ya kijamii,” imefafanua.

“Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara linawaomba ndugu na jamaa wa Anastanzia Exavery Mahatane maarifu kama Ebitoke kufika Mkoa wa Mtwara kutoa msaada au kumchukua ndugu yao,” imesema taarifa hiyo ya polisi.