Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango ameiagiza Wizara ya Uvuvi kuwawezesha vijana wanaofuga samaki kwa kutumia vizimba ili wapate mitaji mikubwa ya kuwawezesha kuyafikia masoko ya kimataifa.
Pia ameiagiza Wizara hiyo kuweka mkakati kabambe wa kuwatangaza kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili wawe ushuhuda kwa vijana wengine wavutiwe na waweze kujiajiri.
Dk Mpango alitoa maagizo hayo leo Ijumaa Agosti 01,2025 wakati alipotembelea maonesho ya wakulima maarufu kama nane nane mkoani Dodoma baada ya kusikia ushuhuda wa vijana wanaofuga samaki.
Vijana hao tisa wa kikundi cha VIJANA NGUVU KAZI MWANZA walikopeshwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili wafuge samaki kwa kutumia vizimba ambao walimweleza namna walivyofanikiwa.
Baada ya kusikia maelezo ya vijana hao, Dk. Mpango amesema vijana hao wanapaswa kutangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kama ushuhuda wa namna vijana wanavyoweza kujiajiri wenyewe.
“Hawa vijana nataka niwaone kwenye vyombo vya habari mara kwa mara kwasababu kuna vijana wengi mtaani wanalalamikia ajira watumieni hawa watakuwa walimu wazuri kwa wenzao waingie kwenye sekta ya ufugaji samaki ambapo wataondokana na umaskini,” amesema
“Mmesikia maelezo yao na hawa hawana changamoto wanachotaka ni kupata nguvu ya kukua kwa kupata mtaji zaidi, benki zingine mpo hapa wasaidieni hawa vijana wapate mtaji mkubwa waweze kuchakata samaki na kuuza hata kwenye masoko ya kimataifa,” amesema
Dk Mpango amepongeza hatua ya vijana hao kusaidiwa mitaji iliyowawezesha kuanzisha biashara mbalimbali ambazo zimewakwamua kiuchumi.
“Minofu ya samaki ina soko kubwa ndani na nje ya nchi kwa hiyo wakiwezeshwa watafanya biashara kubwa sana, nawapongeza sana kwa kuwawezesha vijana hawa mmefanya jambo jema na zuri endeleeni kuwashika mkono ili waweze kukua zaidi,” amesema Dk Mpango
Katibu wa kikundi hicho, Pius Makindi amemwambia Makamu wa Rais kuwa wako vijana tisa na walikabidhiwa mradi huo Januari mwaka jana na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema walianzisha mradi huo baada ya kupata mkopo wa shilingi milioni 137.9 benki ya TADB uliowawezesha kununua vizimba tisa na kuanza kufuga samaki na kufanikiwa kuvuna vizimba sita ndani ya miezi sita walipofanikiwa kupata faida ya shilingi milioni 102.
Amesema walipovuna tena vizimba vitatu vilivyobaki walifanikiwa kupata shilingi milioni 25 na walifanikiwa kurejesha mkopo kiasi cha shilingi milioni 68 na wao wakabaki na milioni 34 ambazo waligawana kuendesha maisha.
Amesema baada ya kufanikuwa kulipa mkopo wa awali walikwenda tena ambapo walikopeshwa tena shilingi milioni 63 ambazo waliziwekeza na kufanikiwa kupata matokeo makubwa ya faida ya shilingi milioni 106.
“Tunatamani sasa tutoke tulipo ili tuchakate samaki na kuuza nje kwa hiyo tunaomba serikali itusaidie kupata mtaji zaidi kwasababu tuko wengi hata tukipata faida tunagawana watu tisa kwa hiyo tunachopata ni kidogo,” amesema
“Tunaomba taasisi za fedha na mashirika watutembelee tuwaeleze mipango yetu ili watukopeshe mtaji mkubwa zaidi tutoke kwenye vizimba tisa twende kwenye vizimba angalau 30 au 50 kwasababu tukiwa na vizimba vingi faida itakuwa kubwa sana na sisi tutakuwa kiuchumi kwa muda mfupi,” amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED