Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Mongela, amesema kuwa uchaguzi wa wabunge wa Viti Maalumu kupitia Jumuiya za chama hicho unafanyika kwa mujibu wa miongozo na kanuni rasmi za chama, na si kwa matakwa au fikra za mtu binafsi.
Mongela alitoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, uliolenga kuwachagua wabunge wa Viti Maalumu kupitia jumuiya hiyo.
“Uzuri wa Chama chetu ni kwamba tayari kilishaweka miongozo yote ya uchaguzi. Hivyo unapokuja hapa kusimamia uchaguzi huu, hutumii akili yako ya kuzaliwa. Niwahakikishie wajumbe wa mkutano huu maalum kuwa tutafuata miongozo na kanuni zote za chama katika mchakato huu,” alisema Mongela.
Mongela, ambaye pia ni msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, alibainisha kuwa kamati ya uchaguzi inayoongoza mchakato huo imejipanga kusimamia kikamilifu taratibu zote za chama, ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na ufanisi.
“Tutahakikisha tunafuata kanuni zote zilizowekwa na chama, na kila hatua ya mchakato itazingatia misingi ya haki. Ni wajibu wetu kuhakikisha uchaguzi huu hauharibiwi kwa sababu ya uzembe au kutofuata taratibu,” alisisitiza.
Kwa lengo la kuimarisha uaminifu na uwazi, Mongela alisema kuwa kura zote zitapigwa na kuhesabiwa ndani ya ukumbi huo huo wa mkutano, mbele ya wajumbe wote.
“Tutahakikisha kura zinapigwa katika ukumbi huu na kuhesabiwa mbele ya kila mtu, ili kila mshiriki awe shahidi wa mchakato mzima. Hili ni jambo la msingi katika kuimarisha demokrasia ndani ya chama chetu,” alisema Mongela.
Alihitimisha kwa kuwataka wajumbe wote kuishi kwa kufuata kanuni za chama hadi mchakato huo utakapotamatika rasmi, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa heshima na mafanikio kwa Jumuiya ya Wazazi na CCM kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED