Wagombea udiwani kata kupigiwa kura za maoni

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:02 AM Aug 01 2025
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla
Picha: Mtandao
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla

Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imeelekeza kwamba wagombea wote wa udiwani waliopitishwa na Kamati za Siasa za mikoa warejeshwe kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni upya.

Katika hatua hiyo, pia imeelekezwa kuwa wagombea wote waliokuwa kwenye orodha ya awali iliyopelekwa kwa makatibu wa CCM wa mikoa yote, nao warejeshwe kwenye mchakato wa kura za maoni.

Taarifa rasmi ya chama hicho kwa umma imeeleza kuwa maamuzi hayo ni matokeo ya kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika Julai 31, 2025, ambapo kilijadili kwa kina malalamiko yaliyowasilishwa kutoka mikoa mbalimbali nchini kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Kutokana na maamuzi hayo, kikao hicho pia kimefuta maelekezo yote ya awali yaliyokuwa yametolewa kuhusiana na uteuzi wa wagombea, na kinawaagiza makatibu wote wa mikoa ya CCM kuhakikisha wanazingatia na kutekeleza maagizo mapya kama yalivyotolewa.