Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Suzan Mkangwa amesema Sekta ya Kilimo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaotumishwa nchini zaidi ya asilimia 84.
Suzan, alitoa takwimu hizo juzi wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa kutokomeza utumikishwaji wa watoto katika sekta hiyo kwa ajili ya kuimarisha sheria za kazi na kulinda haki za watoto nchini.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Hali ya Utumikishwaji wa Mtoto nchini iliyochapishwa mwaka 2024, takriban watoto milioni tano sawa na asilimia 25 wanajihusisha na kazi, huku milioni 4.9 (asilimia 24.3) kwa utumikiswajimbaya wa watoto.
Alisema asilimia 84.1 ya watoto hao wanatumikishwa katika kilimo, hali inayodhihirisha ukubwa wa changamoto inayokabili sekta hiyo nchini.
“Mwongozo huo mpya utasaidia kuongeza kasi ya kutokomeza ajira za watoto kwa kuweka mwelekeo mahsusi kwa wadau wote wa sekta ya kilimo," alisema.
Alisema baada ya uzinduzi huo, mafunzo yatatolewa kwa wadau wa msingi kwa ajili kusambaza mwongozo huo katika ngazi zote za Serikali Kuu na Serikali za Mitaavyo.
Vilevile, alisema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa mwongozo huu kupitia kaguzi, elimu na ushauri kwa wadau wa sekta ya kilimo.
Alifafanua zaidi ya kuwa Mpango Kazi wa kila mdau umeandaliwa ili kusaidia kufuatilia jukumu la kila mmoja na kutoa taarifa sahihi kwa mamlaka husika.
Suzan, alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda haki za watoto na kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanapatikana kwa njia endelevu na salama.
Kwa upande mwingine, aliipongeza Wizara ya Kilimo, Bodi za Mazao Tanzania na Shirika la ECLT kwa kuendeleza utekelezaji wa haki za wafanyakazi hususan katika sekta ya kilimo na tumbaku.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED