Jaji Siyani: Migogoro ya uchaguzi kipimo cha Mahakama kutenda haki

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:43 PM Aug 01 2025
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Mustapher Mohamed Siyani
Picha: Mpigapicha Wetu
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Mustapher Mohamed Siyani

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Mustapher Mohamed Siyani, amesema kuwa migogoro inayotokana na mchakato wa Uchaguzi Mkuu ni kipimo halisi cha uwezo wa Mahakama katika kutenda haki kwa weledi, kasi na bila upendeleo.

Dk. Siyani aliyasema hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji, yaliyofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court), ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

“Mchakato wa uchaguzi na utatuzi wa migogoro yake ni kipimo kwa Mahakama. Majaji mnatakiwa kuwa makini, wenye weledi, maadili, na kutoa uamuzi kwa haki na haraka – pasipo kufungwa na mbinu za kiufundi,” alisisitiza Dk. Siyani.

Dk. Siyani alisema kuwa mchakato wa uchaguzi huambatana na matarajio makubwa ya wananchi, hisia kali za kisiasa, pamoja na mvutano wa kimtazamo baina ya wadau wa demokrasia. Hivyo, alisema, ni wajibu wa Mahakama kuhakikisha mashauri yote ya uchaguzi yanapewa uzito na kipaumbele cha kipekee.

“Ni muhimu kwa majaji kuhakikisha wanashughulikia mashauri ya uchaguzi kwa kasi, kwa haki, na kwa ufanisi, ili kudumisha imani ya wananchi kwa Mahakama,” alieleza.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itawawezesha Watanzania kuchagua viongozi wao kwa njia ya kura na kuendelea kushiriki katika ujenzi wa Taifa kwa amani na utulivu.

Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uwezo wa majaji katika misingi ya kikatiba na kisheria kuhusu uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi nchini.

“Matumaini yangu ni kuwa mafunzo haya yataongeza viwango vya weledi, maadili na kasi ya utendaji kwa majaji wetu,” alisema.

Aliwataka washiriki wote kutumia vyema fursa hiyo kufanya maandalizi madhubuti ya kushughulikia mashauri hayo kwa haki, haraka na bila upendeleo.

Jumla ya majaji 103 wa Mahakama Kuu walishiriki katika mafunzo hayo ya siku moja, yaliyofanyika kwa njia ya mtandao, ikiwa ni mkakati wa kitaasisi kujiandaa kwa changamoto zinazoweza kujitokeza katika kipindi cha uchaguzi.

Dk. Siyani alihitimisha kwa kuikumbusha Mahakama nafasi yake ya kipekee katika kuimarisha amani, utulivu wa nchi na mazingira wezeshi ya ukuaji wa uchumi kupitia utoaji wa haki kwa wakati.