KIVUMBI uchaguzi wa wabunge wa viti maalum ndani ya Jumuiya za CCM kutimka leo kwa wagombea 34 katika Mkutano Mkuu Maalum wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) kusaka wawakilishi kwenye makundi manne.
Makundi hayo ni; wawakilishi wa Watu Wenye Ulemavu, Wasomi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NG’Os) na Wafanyakazi.
Miongoni mwa wagombea watakaochuana ni aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira, Halima Mpinde (Muugizaji wa filamu maarufu jina la Davina), Asha Baraka (kundi NG’Os).
Kundi la wasomi yumo, Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk. Benardetha Rushahu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania Dk. Regina Malima, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya, Dk. Siriel Mchembe, huku kwa Tanzania Zanzibar yumo Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis.
Kundi la watu wenye ulemavu ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa (watu wenye ulemavu).
Kundi la Wafanyakazi yumo, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Alice Kaijage, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’I Mazana Issa na Naibu Katibu Mkuu UWT Taifa, Riziki Kingwande.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, kuhusu mkutano huo, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, aliwataka wajumbe wawashindanishe wagombea kwa hoja na sifa na si kwa fedha au vitu vingine vya kuwashawishi.
“Niwatake wajumbe wote wa mkutano huu. Chama chetu kimeelekeza wazi kuwa kinapiga vita rushwa. Ninajua wagombea wamekuja na wapambe wao. “Tafadhali wajumbe mnapaswa kujiepusha na majaribu ya kupokea fedha kutoka kwa wagombea au wapambe wao. Chagueni viongozi kwa haki na kwa kuzingatia sifa, si kwa sababu ya kupewa fedha au kitu,” alisema Chatanda.
Alisisitiza kuwa suala la rushwa linalaaniwa vikali na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akilipigia kelele mara kwa mara na ameonesha msimamo wake katika kukabiliana na rushwa hivyo UWT iungane naye.
“Sisi UWT tunaungana naye kwa kauli hiyo na tunawataka wajumbe mzingatie haki. Wasichaguliwe watu kwa misingi ya ushawishi wa fedha, bali kwa uwezo wao wa kuwatumikia wanawake wa Tanzania,” alieleza.
Chatanda aliwataka walioongoza kwa kura katika uchaguzi wa UWT uliofanywa katika mikoa wasibweteke kusaka kura za ushindi wa CCM kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani kwa kuwa ndio utakaowapa nafasi ya kuteuliwa ubunge viti maalum.
Alisisitiza uchaguzi utafanyika kwa amani na uwazi na vipaumbele vikiwa ni maadili, uwajibikaji na uongozi bora.
JUMUIYA WAZAZI
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Mongela, jana alifungua mkutano wa uchaguzi wa wabunge wa viti maalum kupitia Jumuiya ya Wazazi na kueleza kuwa unafanyika kwa mujibu wa miongozo na kanuni zilizowekwa na chama na si akili ya mtu binafsi.
"Tutahakikisha tunafuta kanuni zilizowekwa na chama pamoja na miongozo yote, hivyo kwa sasa wajumbe wote tunapaswa kuishi kikanuni hadi mchakato huu utakapomalizika, ili kuepuka kuharibu uchaguzi wetu,"alisema Mongela
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ally Hapi, alisema wako wagombea 33 ambao majina yao yaliteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ambayo yatapigiwa kura na wajumbe kwa ajili ya kupata wabunge wa Viti Maalum.
VIJANA WAFUNDWA
Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohamed Aboud Mohamed, alisema CCM hakitaki viongozi watakaochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, kuwa chanzo cha migogoro ndani ya chama na nchi.
Alisema viongozi wote wenye sifa za migogoro na tabia zisizoridhisha katika chama hawatakiwi, hivyo hawatavumiliwa.
Mohamed alisema katika ndani ya chama kunatakiwa watu safi, kiongozi anayetetea maslahi ya taifa, mtenda haki, mchapakazi, asiyemwoga na anayejua wajibu na mipaka yake katika kazi.
"Vijana ndio Dira ya kusimamia misingi ya uhai wa taifa na kusimamia maendeleo na mafanikio ya nchi, kila litakalotokea hapa likiwa na sura nzuri tutakuwa tumetoa sura ya uzuri wa chama na nchi kwa ujumla.
"Likitokea kosa lolote tutakuwa tumeharibu sura ya chama chetu, hapa tunafanya jambo kubwa kwa maslahi ya chama chetu, hivyo lazima tufanye kazi hii kwa uadilifu na kufuata taratibu zote,"alisisitiza mjumbe huyo.
“Wagombea tunao 58 wamekubalika na chama ndio maana wameletwa kwetu, ili tuwapigie kura za mapendekezo na baadaye chama kitafanya uamuzi wa mwisho.
“Wako watu inasemekana wanapanga matokeo, hilo halitatokea hapa. Wako wenye nia ya kutoa rushwa na wengine wameanza kujitokeza watakuwa wamejiharibia safari yao,” alisema.
Awali, Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwegelo, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuvunja makundi yaliyoko mara baada ya uchaguzi kumalizika, ili kuijenga jumuiya yenye umoja na mshikamano.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED