Mawakili wa Lissu walaani kitendo cha mteja wao kusukumwa Mahakamani

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 04:14 PM Aug 01 2025
Mwanasheria wa CHADEMA, Wakili Dk. Rugemeleza Nshala katikati akizungumza na waandishi wa habari.
Picha: Imani Nathaniel
Mwanasheria wa CHADEMA, Wakili Dk. Rugemeleza Nshala katikati akizungumza na waandishi wa habari.

Mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini na uchochezi, wamelaani vikali kitendo kinachodaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa Magereza cha kumsukuma na kumdhalilisha mteja wao mara baada ya kesi kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, wakiongozwa na Wakili Dk. Rugemeleza Nshala, amesema tukio hilo ni kosa la kisheria, ni kinyume cha utu wa binadamu, na ni fedheha kwa mhimili wa Mahakama.

“Kitendo cha kumsukuma mteja wetu, ambaye ni mlemavu wa kudumu, si tu ni udhalilishaji bali pia ni kuingilia uhuru wa Mahakama. Askari walimzunguka wakiwa wamejifunika nyuso – jambo ambalo halikubaliki kisheria wala kimaadili,” amesema Dk. Nshala.

Ameongeza kuwa tukio hilo linaashiria kuingiliwa kwa mihimili ya dola na kudhoofisha misingi ya haki nchini.

“Tutawasilisha barua rasmi kwa Majaji wa Mahakama Kuu tukitaka askari wa Magereza waliovunja taratibu wawajibishwe. Mahakama ni eneo huru na kila mtu anapaswa kulindwa utu wake – hata akiwa mahabusu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Wakili Mpare Mpoki amesema tayari wameomba kikao rasmi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, wakilenga kujadili namna bora ya kukomesha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watuhumiwa na wafungwa mahakamani.

“Hakuna kifungu chochote cha sheria kinachoruhusu askari kumdhalilisha mtuhumiwa, zaidi hasa anapokuwa mikononi mwa Mahakama. Tunasisitiza kuwa hatua zichukuliwe mara moja,” amesema Mpoki.

Amesisitiza kuwa mawakili kama maofisa wa Mahakama hawatarajii kufumbia macho vitendo vinavyokiuka misingi ya haki na utu.

Wapinga Askari Kufunika Nyuso Mahakamani

Mawakili hao pia wamepinga vikali tabia ya askari kufunika nyuso zao wanapokuwa mahakamani, wakisema ni kinyume cha maadili ya uwazi katika utoaji haki.

“Mahakama ni eneo la uwazi. Askari kufunika nyuso kunazua hofu na mashaka kuhusu dhamira ya matendo yao. Tunataka uwajibikaji na uadilifu mahakamani,” walisema kwa pamoja.

Tundu Lissu bado anasubiri kuendelea kwa kesi yake, huku suala la haki na usalama wake likizidi kuibua mijadala kuhusu mwenendo wa vyombo vya ulinzi ndani ya mazingira ya Mahakama.