KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), imeridhika na ujenzi wa jengo la Mama na mtoto katika Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, likiwa na uwezo wa kubeba vitanda vya wagonjwa 148 kwa wakati mmoja.
Jengo hilo linajengwa na Mkandarasi Suma JKT ya mkoani Geita, kwa Sh. bilioni 6.79 fedha kutoka mapato ya ndani ya Manispaa ya Kahama na ulianza Julai 15, mwaka 2022 linatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga, ametoa pongezi hizo leo, baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa jengo hilo kutoka kwa Meneja wa Mradi, Mashala Mboje.
"Jengo hili sisi tumeridhika nalo kabisa na tunampongeza Mkurugenzi wa Manispaa hii, kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha za kuanzisha ujenzi wake. Tunazitaka Halmashauri nyingine kuiga mfano huu, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi," ameongeza.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinganga (CHADEMA), Salome Makamba, ameipongeza serikali kwa kujenga jengo hilo ambalo litakuwa pia na kitengo cha huduma kwa watoto njiti na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED