UMOJA wa Vijana wa CCM Mkoa wa (UVCCM) Shinyanga, umesema umewafikia wanachama zaidi ya 169,426 na kuwasajili kwa njia ya kieletroniki kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka.
Mwenyekiti wa UVCCM mkoani wa Shinyanga, Bernad Werema, ameyasema hayo, leo, wakati wa kikao maalumu cha kujadili masuala ya kujenga umoja huo,kilichofanyika Manispaa ya Kahama na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mabala Mlolwa kama mgeni rasmi.
Amesema, wametekeleza agizo la chama la kutaka wanachama kusajiliwa kwa njia ya kieletroniki na kati ya waliosajiliwa 89,820 ni wanaume na 79,667 wanawake.
Werema amesema, mchakato utakuwa endelevu kila mwaka kwa sababu kwenye umoja wao, kila mwaka wamekuwa wakiongeza vijana, hivyo watakuwa wanawafikia na kuwasajili ili kuongeza nguvu kazi ya chama na kuwasisitiza wale wanaosoma kuongeza juhudi katika masomo yao.
"Sisi vijana tumeazimia kwa kauli moja kuunga mkono azimio la mkutano mkuu maalumu wa CCM uliofanyika Januari 18 na 19 mwaka huu, 2025, jijini Dodoma lililopitisha wagombea urais Tanzania bara na Visiwani uchaguzi mkuu mwaka huu, tutatafuta kura zao mpaka watashinda kwa kishindo," amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewapongeza kwa hatua ya kuwafikia wanachama wao, kuwasajili na kuhakikisha wanalipa ada na kuwataka kuwa wamoja katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Amesema, joto la uchaguzi linasababisha baadhi ya wanachama kuondolewa kwenye ngazi zao hasa zile za chini, mashina na matawi, kwa sababu viongozi wanaambiwa ukweli au kukosolewa na kuwaomba kuvumiliana kwa makosa yanayojitokeza, ili kukijenga chama
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED