KUELEKEA kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli, Machi 17, 2025, maelfu ya Watanzania wamejitokeza kwenye matembezi ya amani kumuenzi kwa mambo makubwa aliyotekeleza enzi za uhai wake.
eMbali na matembezi hayo, familia ya Hayati Dkt. Magufuli imetoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Rufaani ya Kanda Chato (CZRH) ikiwa ni matendo ya huruma kwa wahitaji.
Katika matembezi hayo yenye umbali wa takribani kilomita tatu yaliyoratibiwa na familia kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), yamewahusisha watu mbalimbali ikiwamo baadhi ya viongozi wa serikali, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo.
Wakiwa katika CZRH, wamempongeza Hayati Rais Magufuli kwa maono yake ya kuanzisha miradi mikubwa ya kitaifa ikiwamo ujenzi wa hosptali hiyo, ambayo kwa sasa inahudumia wagonjwa zaidi ya 40,000 kwa mwaka.
Imeelezwa kuwa kabla ya uwepo wa hospitali hiyo,wananchi walikuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za matibabu ya kibingwa na ubobevu kupitia hospitali ya Bugando Mwanza na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Dk. Magufuli, mtoto wa marehemu Jesca John Magufuli, amesema familia hiyo inaungana na watanzania wote kuelekea kumbukizi ya kifo cha mzazi wao kwa kutoa matendo ya huruma kwa wagonjwa wenye uhitaji.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake kubwa ambazo ameendelea kuzionesha kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na kuendeleza mema yote yaliyoachwa na mtangulizi wake.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika matembezi hayo, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ( UVCCM), Rehema Sombi, amedai kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na Hayati Magufuli, katika ujenzi wa hospitali hiyo ambayo imekuwa kimbilio la wagonjwa kutoka nchi za DRC, Rwanda, Uganda na Burundi.
Kadhalika amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kukamilisha miradi mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake na kwamba utekelezaji huo ni mafanikio makubwa ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali CZRH, Dk. Osward Lyapa, amesema uwepo wa huduma za kibingwa na bobezi kwenye hospitali hiyo umesaidia sana jamii kupata huduma bora na za uhakika katika maeneo yaliyo karibu yao ukilinganisha na awali walipokuwa wakilazimika kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Machi 17, kesho, Ffamilia ya Hayati Dk. Magufuli itaungana na Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, kuadhimisha Misa maalumu ya kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha mzazi wao, aliyekuwa Rais wa Tanzania, kabla ya kukumbwa na umauti wakati akipatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED