Mradi wa umwagiliaji wa bilioni 6.4 waanza Kijiji cha Nambalapi

By Stevie Chindiye , Nipashe
Published at 04:07 PM Mar 16 2025
Mradi wa umwagiliaji wa bilioni 6.4 waanza Kijiji cha Nambalapi
Picha: Mpigapicha Wetu
Mradi wa umwagiliaji wa bilioni 6.4 waanza Kijiji cha Nambalapi

Serikali imezindua ujenzi wa mradi mkubwa wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Nambalapi, Kata ya Masonya, Wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma.

 Mradi huo, unaokadiriwa kuwa na gharama zaidi ya shilingi bilioni 6.4, unatarajiwa kuboresha sekta ya kilimo na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.  

Diwani wa Kata ya Masonya, Said Beansli, ametoa wito kwa wananchi wa eneo hilo kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika mradi huo ili kuhakikisha  malengo yake yanafikiwa. 

Amesema kuwa mradi huo ni fursa muhimu ya kukuza uzalishaji wa kilimo, kuongeza kipato cha wakulima, na kutatua changamoto za ukame zinazowakumba wakulima wa eneo hilo.  

Kwa mujibu wa serikali, mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo nchini na kutatua changamoto za ukame zinazokabili maeneo kadhaa ya nchi. Ufanikishaji wake katika Kijiji cha Nambalapi unatarajiwa kuwa kioo cha mafanikio kwa maeneo mengine yanayokabili changamoto sawa.