TRA yawahimiza wananchi kudai risiti na kulipa kodi kwa hiari

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 08:22 PM Mar 15 2025
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka waislamu na wakristo kwa kipindi hiki cha mfungo mtukufu wanaweza kuichangia nchi kwa kuhakikisha kila wanachonunua wahakikishe wanadai na kupewa risiti kwa sababu matumizi wanayofanya sasa ni ya kununua bidhaa.

Aidha, imesema itahakikisha hawachukui kisichostahili kuchukuliwa, lakini itahakikisha haiachi kinachostahili kuchukuliwa kutoka kwa walipa kodi.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda katika hafla ya Iftari iliyoandaliwa na TRA jijini Dar es Salaam ikiwakutanisha wafanyabiashara, watumishi wa TRA na wadau mbalimbali wa masuala ya kodi.

Amesema lengo ni kuwashukuru na kuwahimiza waendelee kulipa kodi kwa hiari, aliwahakikishia kwamba kwasababu wamepewa dhamana kusimamia ukusanyaji wa kodi wataitenda kwa haki.

"Tutahakikisha hatuchukui tusichostahili kuchukua lakini tutahakikisha hatukiachi tunachostahili kuchukua kutoka kwenu,"amesema Kamishna Mwenda 

Aidha, amesema wanautaratibu mzuri kwa walipa kodi kutoa taarifa kama kuna baadhi ya watumishi hawaendi vizuri katika utendaji wao wa kazi.

Pia, amesema viongozi wa dini wamezungumza kuhusu mahusiano ya kodi na uislamu na wamesema kama kodi inayokusanywa inakwenda kwa manufaa ya wananchi basi hiyo ni halali.

, Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Sheikh Ally Hamis Ngeluko

"Kwa hali hii ni  halali kwa imani zetu kulipa kodi kama ni halali ni halali pia kuwahimiza tulipe kodi, lakini wakati tunawashukuru kulipa kodi tuombe pia muendelee kulipa kodi kwa hiari na hata katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu Kwaresma na Ramadhani,"amesema 

Kwa upande wake, Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Sheikh Ally Hamis Ngeluko amewataka wananchi kulipa kodi kwa hiari na kwa uaminifu kwa sababu ndiyo maendeleo ya nchi yanapotokea huko.

Pia, amesema nchi haijengwi kwa udongo bali kwa mapato hivyo watoto wakijengewa utamaduni wa kulipa kodi kama ilivyo kwa wazazi wao nchi itaendelea kujengwa kwa maendeleo ya Taifa.

"Niwahimize watanzania wenzangu tuwarithishe watoto wetu wawe na utamaduni wa kulipa kwa hiari ili watakapokuwa wakubwa wawe walipokodi watakaoijenga nchi yetu,"amesema Sheikh Ngeluko