HUYU NDIYE TABITHA SIWALE; Mtoto wa mkalimani, aliyepiga kikumbo vikwazo vya msichana

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:02 AM Mar 15 2025
Tabitha Siwale
Picha: Mtandao
Tabitha Siwale

TABITHA Siwale, ni miongoni mwa wanawake wa kwanza kuwamo kwenye Baraza la Mawaziri chini ya Rais Mwalimu Julius Nyerere.

Alikuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi wa kwanza mwanamke.

Kifo chake mwishoni mwa wiki, kimeacha alama kwenye jamii ya Kitanzania hasa kwa wasichana na wanawake.

Aliwahi kuwa Waziri wa Elimu kwenye serikali ya awamu ya kwanza, akisema kuwa miaka ya elimu yao, mwamko wa elimu kwa wasichana ulikuwa mdogo tofauti na miaka ya hivi sasa.
Alishika nyadhifa tofauti 1975-80 ‘Minister of Housing and Lands’ na 1980-82 ‘Minister of National Education.’

Miongoni mwa tabia zake ni kupenda kulala mapema; “Hii inanifanya niamke usiku muda wowote na kusoma  kwa kuwa ni lazima nisome na nilipokuwa kiongozi.

“Siwezi kwenda katika mkutano na kuacha kupitia ’document’ mbalimbali, ili niwe na ‘background’ ya kitu nitakachozungumzia au kukisikiliza.”

Anasema kwamba elimu kwa mtoto wa kike miaka hiyo, haikuonekana kuwa na manufaa wakati huo jambo lililoifanya serikali kutumia nguvu kubwa kuhamasisha jamii kusomesha watoto wa kike.

Aidha, alieleza kuwa mfumo wa elimu unaotolewa hivi sasa katika serikali ya awamu ya tano ikiwamo elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, kwamba umechangia ongezeko la mwamko huo.

Siwale alibainisha hayo, Februari, mwaka 2017, alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na mwandishi wa makala hii.

Mwaka huo alikuwa na umri wa wakati huo miaka 76, akiwa nyumbani kwake katika mahojiano maalum, Msasani, Dar es Salaam, alipolezea kuhusu masuala mbalimbali ya elimu ikiwamo mafanikio, changamoto na nini kifanyike, ili kuendeleza elimu nchini.

Alisema kwa kipindi hicho (mwaka 2017), alikuwa anasimamia shughuli za biashara ambazo hazihitaji kuumiza kichwa kwa kuwa tayari amekwishakuwa mtu mzima sana.

Alisema kwamba hatua ya elimu iliyofikiwa nchini, inahitaji kuwa na manufaa kwa wote kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho huku akigusia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), izingatie urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika, ili iwanufaishe na wengine.

“Nasikia sasa hivi kuna bodi ya mikopo kwa ajili ya wanafunzi, inapaswa watu wakiwa waaminifu, wakiirejesha mikopo hiyo kwa wakati itaifanya bodi iwe hai, lakini kama si waaminifu waliokopeshwa itakuwa si endelevu, malengo hayatafikiwa,” alisema Siwale na kuongeza…

“Zamani tulikuwa hatukopeshwi, kulikuwa hakuna bodi tulikwenda vyuoni moja kwa moja, lakini sasa bodi hii isaidie kweli vijana.”
Siwale aliwashawishi wasichana na wanawake wanaojiendeleza kielimu, kuweka nia na kuzingatia masomo kwa wakati bila kupoteza muda.

“Unapofundishwa ‘listen’ na ukifundishwa soma, hakuna kitu kinachokuja mkononi au mezani ni juhudi, nilipenda kusoma sana niliamka hadi usiku yaani muda wowote nisome, na hata nilivokuwa waziri nilikuwa lazima nipitie ‘documents’ mbalimbali ili zinipe mwongozo na kuniongezea uelewa wa suala lililo mbele yangu.

Alifafanua namna elimu inavyoweza kuchangia maendeleo ya taifa pamoja na kuliinua kundi la wasichana/wanawake ambao wataitumia vyema elimu yao.

ASILI YAKE

Siwale kwenye mahojiano hayo, alisema kuwa asili yao nyumbani kwa wazazi wake ni Bagamoyo mjini, Tukuyu, mkoani Mbeya.
Baba yake (Wilfred Mwambenja) alikuwa ni mchungaji na wakati huo huo alikuwa mkalimani.

Ukalimani wa lugha hulenga kurahisisha mawasiliano ya lugha ya mdomo au lugha ya alama kati ya watumiaji wa lugha mbili tofauti.

Anasema historia anayoikumbuka akiwa mdogo, ni kwamba babu yake (upande wa baba) alikuwa anapenda kufanya mawasiliano na wakoloni na walimshawishi kuwasomesha watoto wake shule ya Malangali.

“Baba yangu alikuwa akiwasiliana na wakoloni na walimtumia katika shughuli mbalimbali aliwasaidia mambo mengi hivyo ni kama walimzawadia na kutoa fursa kwa watoto wake, akiwamo baba yangu wakasome, hivyo baba yangu ni kati ya wasomi wanyakyusa wa kwanza,” anasema Siwale.

Anasema baba yake baada ya kusoma alikuwa ni mkalimani wa lugha moja kwenda nyingine, aidha kutoka lugha ya kiingereza kwenda kinyakyusa au kiingereza kwenda Kiswahili na kufikisha ujumbe katika hadhira.

“Baadae alipohamia Mbeya mjini, alikwenda hadi kuwa mkalimani katika mabaraza ya mahakama.”

Haya ni miongoni mwa maswali aliyoulizwa wakati huo;

Swali: Je ulipata wapi ujasiri wa kushika ngazi ya uongozi kitaifa ikizingatiwa ulikuwa mwanamke?

Jibu: Nilipata ujasiri nilishirikiana na wenzangu katika wizara ya elimu, elimu ilitolewa bila ubaguzi na wote walionekana sawa mbele ya serikali. Nilikuwa sikubali kushindwa katika utekelezaji wa majukumu yangu eti kwa kuwa ni mwanamke.

Swali: Kwa nini unasema mwamko wa elimu ulikuwa mdogo kipindi hicho hasa kwa wasichana?

Jibu: Idadi ya wasichana shuleni ilikuwa ndogo, tulitakiwa kuhamasisha na kuwaambia wazazi, walezi eti kwa mtoto wa kike ni haki, utakuta mzazi anasema asisome aolewe, tuliwaambia kuolewa ataolewa lakini asome kwanza, kwa hiyo hata idadi ya wasichana darasani ilikuwa ndogo.

Wazazi walifikiri kusomesha ni mvulana tu, mahudhurio yalikuwa ni madogo katika uandikishaji, wazazi walihitaji msukumo.
Swali: Iwapo ungekutana na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia (wakati huo Prof. Joyce Ndalichako), Je, ungemshauri nini au uzoefu gani ikizingatiwa kwamba ulikuwa waziri kama yeye?

Jibu: Kwanza ningempongeza na kumtakia kila la kheri, najua ameonekana anafaa na kujifunza ukiwa utekeleza vizuri zaidi na kufuata taratibu, lakini ningeshauri kutokimbilia sana kuanzisha kitu kipya ukidhani ni kizuri, angalia kwanza yaliyofanyika nyuma yalikuwa ni kwa nia nzuri, lakini kuwe na uaminifu wa kuyatekeleza hayo yanayopangwa.

Swali: Unaonaje mfumo wa elimu bure nchini?

Jibu: Hii imechangia idadi ya wanaojiunga na shule kuongezeka, nampongeza Rais Magufuli (wakati huo), kwa uamuzi huo.
Zamani tulikuwa hatukopeshwi, kulikuwa hakuna bodi tulikwenda vyuoni moja kwa moja lakini sasa, bodi hii isaidie kweli vijana.

SIWALE MAISHANI

Siwale aliiambia Nipashe kwamba ni mama wa watoto wanne, akisema pamoja na mwamko mdogo wa elimu kwa watoto wa kike miaka hiyo, alipenda kusoma na kutaka kufanikisha malengo yake aliyojiwekea.

Anasema alisoma Shahada yake ya Kwanza (Bch.Home Economics) katika chuo Kikuu Nairobi nchini Kenya.

Aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum na kisha kuteuliwa kuwa Waziri katika Elimu, nafasi ambayo ilimpasa kuhamasisha jamii kuwasisitiza watoto wao wa kike kujiunga shule.

ATUZWA

Mwaka 2017, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, (sasa Rais), akifungua Tamasha la 14 la Jinsia lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), aliwakabidhi tuzo wanawake waliopigania haki za wanawake tangu uhuru, walioonesha mchango wao katika ukombozi wa haki za wanawake, akiwamo Waziri wa Elimu wa kwanza, Tabitha Siwale.

Wengine waliotuzwa ni pamoja na Prof. Ruth Meena, Anna Abdallah na Prof. Ester Mwaikambo.

WANAWAKE WALIOSHIKA NYADHIFA TANZANIA

Unapoitaja Tanzania na mafanikio yaliyofikiwa sasa, kiuchumi, kijamii na kisiasa, huwezi kukosa kuwataja wanawake ambao walishirikiana bega kwa bega katka ukombozi wa mwanamke.

Upo usemi usemao palipo na maendeleo hakosekani mwanamke nyuma yake.
Bibi Titi Mohamed ni Kati ya kina mama hao na Waziri wa Elimu wa kwanza mwanamke, kwenye Baraza la kwanza la mawaziri, Tabitha Siwale ni miongoni mwao.

GETRUDE MONGELLA

Getrude Mongella alishika nyadhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa, miaka 1993 hadi 1995 alikuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa (AU) wa masuala ya wanawake na kuhudhuria mkutano wake wa nne uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.

Kadhalika aliwahi kuwa balozi wa Tanzania, nchini India mwaka 1991 hadi 1993.
Mongella, pia alikuwa waziri asiye na Wizara Maalum, Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii, mshauri maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO).

ASHA-ROSE MIGIRO

Pia Asha-Rose Migiro aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN, kuanzia Januari mwaka 2007, akipewa cheo hicho na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-Moon.

Aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia Januari mwaka 2006 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Waziri wa Katiba na Sheria pia mbunge wa viti maalumu.

Migiro ana shahada ya uzamili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pia ana shahada ya udaktari kutoka Chuo kikuu cha Konstanz, Ujerumani.

ANNE MAKINDA

Anne Makinda, spika mstaafu pia alikuwa mbunge wa jimbo la Njombe Kusini.
Alikuwa spika kuanzia mwaka 2006 hadi 2010. Na mwaka 1990 na 1995 alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.