Mradi wa maji wa Sh.bilioni 44 halmashauri ya Ushetu kukamilika mwezi Oktoba mwakani

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:51 PM Mar 14 2025
MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita
PICHA: SHABAN NJIA
MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amefanya ziara ya ukaguzi katika mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria unaojengwa kutokea Manispaa ya Kahama mpaka Halmashauri ya Ushetu ukiwa na urefu wa kilometa 68.2.

Mradi huo una thamani ya Sh.bilioni 44 na kwa awamu ya kwanza baada ya kukamilika kwake utahudumia wananchi wa vijiji 54 kwenye kata 11 kati ya 20 zilizopo halmashauri hiyo.

Kadhalika, mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Sihotech Engineering Co.ltd ya jijini Dar es Salaamu kwa kushirikiana na Kampuni ya Mpole Construction and Co.ltd ya Iringa na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka 2026.

Mhita amesema,ni muhimu kwa kila mwananchi kuchukua jukumu la kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, pindi mradi utakapokamilika na itakuwa imesaidia kutokutumia maji yasiyo safi na salama.

“Mradi huu unalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia huduma ya maji ya kutosha na safi, na ni jukumu letu kuhakikisha kuwa unatekelezwa kwa ufanisi" amesema Mhita.

Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, viongozi wa eneo, na wananchi katika kuhakikisha kuwa mradi huo unafaidisha jamii nzima. Alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na wataalamu ili mradi uweze kuleta manufaa halisi kwa wote.

Ziara hiyo ya ukaguzi ilikuwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unatekelezwa kwa ufanisi na unaleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi wa Wilaya ya Kahama.