KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imelipongeza Shirika la Reli Nchini (TRC) kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), pamoja na maboresho ya miundombinu ya shirika hilo.
Kamati hiyo imeitaka Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) pamoja na shirika la Reli (TRC) kuanza kutekeleza mpango wake wa kuunganisha njia ya reli na bandari ya Tanga ambapo kukamilika kwake kunatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Suleiman Kakoso alipofanya ziara ya kukagua na kutembelea miradi ya upanuzi wa bandari leo , uwanja wa ndege pamoja na maboresho ya reli ya mkoani hapa ameipongeza serikali kwa maboresho yanayofanyika katika miradi hiyo.
"Tumefurahishwa na mipango ya baadaye ambayo sasa mamlaka ya bandari inafikiria kwenda mbali zaidi muanze kuweka mifumo ya kuunganisha reli na bandari ili tuwe na miradi mikubwa"
Aidha ameipongeza serikali kupitia Wizara ya ujenzi na uchukuzi ambayo imeanza michakato ya ujenzi wa reli za kisasa katika maeneo mbalimbali nchini ambayo utakapo kamilika itafungua fursa mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.
"Kitendo cha kuanza kufikiria kujenga reli za kisasa mikoani itasaidia sana kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi wetu,tunashauri serikali iwe inashirikisha wawekezaji katika ujenzi wake" alisema Kakoso
"Pamoja na uwekezaji mkubwa ambao mnaweka kwenye shirika la reli, bunge linashauri ni vyema uwekezaji wenu uende sawa na vitendea kazi ili uwekezaji uwe na tija" alisema.
Alisema mkoa wa Tanga unaendelea kufunguka kupitia fursa mbalimbali ikiwemo za kiuchumi katika utekelezaji wa miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara, ukarabati wa reli sambamba na ujenzi wa barabara ya Tanga hadi Singida pamoja na ile ya Tanga hadi Bagamoyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi uendeshaji kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) Focus Sahani ameeleza kuwa wameendelea kuhakikisha usafiri wa njia hiyo unaimarika ambapo hadi kufikia sasa kila wiki ya siku nne wanatoa huduma ya safari za treni za abiria kutoka Dar es salaam,Korogwe Moshi na Arusha.
"Tumepata pongezi kubwa sana kuhusu uanzishwaji wa treni ya kisasa ya SGR pamoja hiyo lakini tuna treni yetu ya MGR tunatoa huduma ya treni ya abiria katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini kila wiki tuna safari nne za treni tangu tulipoifungua hiyo reli, kila tunapofika kuanzia Mwezi Novemba mpaka Februari huwa tunaongeza za treni zinakuwa sita kwa wiki kwa ajili ya kuwahudumia watanzania" alisema Sahani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED