Bunge laitaka Wizara ya Ujenzi kumsimamia mkandarasi barabaraTanga-Pangani-Bagamoyo

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 05:25 PM Mar 14 2025
Bunge laitaka Wizara ya Ujenzi kumsimamia mkandarasi barabaraTanga-Pangani-Bagamoyo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Bunge laitaka Wizara ya Ujenzi kumsimamia mkandarasi barabaraTanga-Pangani-Bagamoyo.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inamsimamia mkandarasi anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Saadani hadi Bagamoyo, ili mradi huo ukamilike ifikapo Juni 16 mwaka huu, baada ya kuongezewa muda wa miezi minne.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Kakoso, alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Tanga - Pangani, kipande cha kilomita 50, pamoja na Daraja la Mto Pangani.

"Naomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe mkataba uliowekwa unaheshimiwa na mkandarasi anasimamiwa ipasavyo ili mradi huu ukamilike kwa wakati. Wananchi wanahitaji kunufaika na miundombinu hii kwa maendeleo yao," alisema Kakoso.

Kwa upande wake, mkandarasi anayetekeleza mradi huo alieleza kuwa ucheleweshaji wa ujenzi umetokana na changamoto ya upatikanaji wa jiwe lenye sifa zinazokidhi viwango vya teknolojia mpya ya lami. Alisema mawe yanayohitajika kusaga kokoto yanapaswa kuwa na nguvu za viwango vya juu.

"Mawe hayo yamepatikana wilayani Muheza, umbali wa kilomita 60 kutoka eneo la mradi. Hata hivyo, yalikuwa na hati miliki za watu binafsi, lakini suala hilo tayari limeshughulikiwa. Hadi sasa, mkandarasi ameshakamilisha kilomita 15.8 za barabara, huku kilomita 34 zikiwa bado. Kwa mujibu wa mkataba, mradi huu unatakiwa kukamilika ifikapo Juni 16, 2025," alisema mkandarasi huyo.