TCRA yataka vyombo vya habari kuripoti uchaguzi bila upendeleo vyama vya siasa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:19 PM Mar 14 2025
Meneja wa Kitengo cha Utangazaji TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka
PICHA: SHABANI NJIA
Meneja wa Kitengo cha Utangazaji TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevitaka vyombo vya habari nchini katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu kuvipatia vyama vya siasa nafasi sawa katika kuripotiwa habari bila upendeleo ili kuondoa malalamiko.

Meneja wa Kitengo cha Utangazaji TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka ameyasema haya leo katika Mkutano wa Misa Tanzania na Wadau (MISA-TAN - Wadau Summit 2025) uliofanyika jijini Dodoma, Mhandisi Kisaka amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa usawa, haki na uadilifu, hasa wakati wa kuripoti habari za vyama vya siasa.

Amesema, kuvipatia haki sawa vyama vya siasa itasaidia kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na zinazowawezesha kufanya uamuzi wa busara hususani wa kuchagua viongozi wanaowataka na sio kukipatia chama kimoja muda mrefu wa kujieleza na kuvinyima vingine, kwani ni kosa kisheria na hatua za kinidhani zitachukuliwa.

"Tujifunze kutenda haki na usawa katika vyama vyote vya siasa, tuwape nafasi sawa, tuwe na usawa katika kuripoti. Tusiweke chumvi na utani, ripoti vile ulivyoona, hivyo ilivyokuwa, usizushe kitu ambacho hakikuwepo. Pia turipoti sera za vyama vya siasa badala ya kujikita kwenye matukio pekee", ameeleza.

Pia amesema wameshtushwa na maombi mengi ya wanasiasa kutaka kumiliki vituo vya redio, huku vingi vikianzishwa kwa ajenda za kisiasa na wananchi kuachwa njiapanda.

Kadhalika, amewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuzingatia maadili ya uandishi na utangazaji wakati wa kipindi cha uchaguzi na kutojihusisha kutangaza matokeo kabla tume ya uchaguzi haijatangaza na wale watakaobainika kufanya hivyo watawajibishwa.

Mhandisi Kisaka amewataka waandishi na watangazaji kutoandika wala kutangaza habari ambazo hazina ukweli na hazina uwiano wowote. Pia wanapaswa kuzingatia kuripoti sera na ahadi za vyama vya siasa, badala ya kujikita zaidi katika matukio pekee. Hii itasaidia kuelimisha umma kuhusu mipango ya vyama na jinsi wanavyokusudia kutatua changamoto zinazowakumba wananchi.