Mahakama yamaliza mgogoro wa ardhi wa miaka 20

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:18 AM Mar 14 2025
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi
PICHA: MTANDAO
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi imemaliza mgogoro wa zaidi ya miaka 20 uliohusisha umiliki wa nyumba ya mjane aliyekuwa Mtaalamu wa Shirika la Maendeleo la Taifa, Regina Ishemwabura (75), aliinunua kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mwaka 1973.

Uamuzi huo umetolewa hivi karibuni na Jaji Elinaza Luvanda dhidi ya walalamikiwa Nasor Hamis, John Mwanga na Fisha Mashoo, baada ya kumtangaza mjane Regina, kuwa ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo ya makazi iliyopo Kiwanja namba 705  bloku ‘F’ iliyotambulika awali kuwa ni nyumba iliyopo Kiwanja namba 94A Drive Inn Cinema, Msasani.

Mahakama imemwamuru dalali, Joshua Mwaituka, anayefanya shughuli hizo kupitia Fosters Companies Ltd, kuwafukuza wadaiwa hao na kuwaondoa mara moja katika nyumba hiyo, iliyopo kando ya barabara ya Bagamoyo.

Aidha, Mahakama imemuagiza dalali wa Mahakama hiyo kuondoa mabadiliko yote yaliyofanywa na wadaiwa bila kuathiri nyumba na kuwafukuza kwa kuvunja nyumba tajwa ili kumwezesha mmiliki halali, Regina kuingia ambae ni mjane.

"Naamuru kurudishwa hati hii siku au kabla ya Aprili 10, 2025, ikionesha namna amri hii imetekelezwa au kushindwa kutekelezwa,’ inasomeka sehemu ya amri hiyo  iliyosainiwa Machi 10, 2025 na Naibu Msajili, Mwajuma Lukindo.

Katika hukumu yake, Jaji Luvanda alipitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Mlalamikaji na kujiridhisha kuwa  Regina ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo iliyopo Kiwanja namba 705 kitalu ‘F’ ambayo awali ilitambulika kuwa ni nyumba iliyopo Kiwanja namba 94A Drive Inn Cinema Msasani kando ya Barabara ya Old Bagamoyo.

Miongoni mwa ushahidi uliotolewa ni pamoja na wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, kumthibitisha mlalamikaji kuwa ni mmiliki halali wa nyumba hiyo na ushahidi wa Benki ya Rasilimali Tanzania, ambapo alipata mkopo wa kununua nyumba na ripoti ya uchunguzi wa polisi juu ya madai ya kughushi, ambayo pia ilionesha kuwa hakuwa na hatia.

'Kwa maoni yangu, kesi ya Mlalamishi iliwasilishwa vizuri na ushahidi uliotolewa ulithibitisha kuwa ana hati miliki nzuri juu ya mali hiyo. Kwa ushahidi mwingi na ripoti hiyo, haishangazi ilikuwa ndiyo sababu ya Nasor Hamis alikwepa kujitetea,' Jaji Luvanda alisema.

Wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, John Mwanga na Fisha Mashoo hawakufika mahakamani wala kuwasilisha hati ya utetezi kwa maandishi, hivyo shauri hilo liliendelea bila pande zote mbili kusikilizwa.

Hata hivyo, maelezo ya maandishi ya utetezi ya Nasor Hamis yalikataliwa baada ya kukaidi kuwasilisha maelezo ya mashahidi kama ilivyoamriwa Machi 5, 2024 na kukataa kuhudhuria tarehe na wakati ambao walipaswa kujitetea.

Mlalamikaji anadaiwa kununua nyumba hiyo kutoka kwa Shirika la Nyumba la Taifa chini ya mpango wa ununuzi wa upangaji ulioendeshwa na Benki ya Nyumba Tanzania (THB).

Ilidaiwa na mdai kuwa baada ya kununua, alikaa katika nyumba kuanzia 1973 hadi 1976 alipohamia Nairobi kuungana na mumewe, na kuacha nyumba chini ya ulinzi wa rafiki yake, Pucharis Kashaija.