Baadhi ya vyama vya siasa nchini vimesema havina mpango wa kususia Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa kigezo cha marekebisho ya Katiba, na kwamba suala la "No Reform, No Election" ni msimamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pekee, si wa vyama vyote vya upinzani.
Kauli hiyo imetolewa mjini Morogoro na Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa.
"Tutashiriki uchaguzi mkuu kama ulivyopangwa, na suala la 'No Reform, No Election' ni la CHADEMA pekee, si la vyama vyote vya upinzani kama inavyodhaniwa," amesema Selasini.
Selasini amefafanua kuwa chama chochote cha siasa kimeanzishwa kwa lengo la kushika dola kupitia sanduku la kura, na hivyo ni wajibu wa vyama kushiriki uchaguzi ili kupata nafasi ya kushinda na kuunda serikali.
"Lengo la kuwa na chama cha siasa ni kushika dola. Sasa utaishikaje hiyo dola kama unakataa kushiriki uchaguzi?" amehoji.
Aidha, amesisitiza kuwa badala ya kutumia nguvu kuhamasisha kususia uchaguzi, vyama vinapaswa kuhimiza wananchi kushiriki kwa wingi ili kuongeza uwakilishi wao bungeni, jambo ambalo litaongeza uwezekano wa kupatikana kwa Katiba mpya.
"Ni kama tunajisahau. CCM ina viti vingi bungeni, sasa tunataka Katiba mpya lakini tunaacha nafasi za kuchaguliwa kwa wingi? Tukisusia uchaguzi, nani atapitisha hiyo Katiba tunayoiomba?" amesema Selasini.
Selasini ameongeza kuwa mchakato wa kupata Katiba mpya unahitaji muda na unapaswa kuwa shirikishi.
"Katiba si mali ya chama fulani bali ni ya wananchi wote. Hivyo, ni muhimu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko badala ya kususia," amesisitiza.
Aidha, amemtaja Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wasira, akisema kuwa alipoteuliwa alisema jambo la kwanza atakaloshughulikia ni maridhiano, na tayari Baraza la Vyama vya Siasa limekuwa kiunganishi kati ya vyama vya siasa na serikali katika kufanikisha hilo.
"Tunashangaa kuona chama kimoja kinatangaza kususia Baraza la Vyama vya Siasa kwa madai kuwa ni muhuri wa serikali, wakati baraza hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mazingira ya siasa nchini," amesema Selasini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema kuwa Watanzania wanahitaji amani na utulivu, na hivyo baadhi ya vyama vya siasa vinavyotoa matamko yasiyo na msingi vinapaswa kuelekezwa jinsi ya kuwasilisha hoja zao kwa njia sahihi.
"Miaka ya nyuma siasa zetu zilikuwa na wigo mdogo, lakini kupitia baraza hili, tulishauri serikali na sasa wigo wa kisiasa umeongezwa," amesema Doyo.
Naye Katibu Mkuu wa Democratic Party (DP) na Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa na Bunge ya Baraza la Vyama vya Siasa, Abdul Mluya, amezungumzia waraka uliotolewa na ACT Wazalendo wakidai kuwa baraza hilo lipo kwa ajili ya kusaidia serikali.
Amesema ACT Wazalendo wanapaswa kuangalia walipotoka na mchango wa baraza hilo katika kuwasaidia kupata nafasi ya kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
"Kabla ya kutoa matamko, ACT Wazalendo wanapaswa kutathmini walikotoka hadi kufika hapa walipo. Wao bado ni chama kichanga, na baadhi ya matamko yao hayako sawa," amesema Mluya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED