Mifumo rafiki ya upatikanaji wa nyaraka iwekwe kuwafikia wananchi kwa wakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:37 PM Mar 13 2025
Mifumo rafiki ya upatikanaji wa nyaraka iwekwe kuwafikia wananchi kwa wakati.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, ameitaka Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuhakikisha mifumo mizuri ya usambazaji wa nyaraka za wazi inaboreshwa ili wananchi waweze kunufaika na taarifa hizo kwa njia ya kidigitali na pia kupitia nakala ngumu.

Lukuvi alitoa agizo hilo leo Machi 13, 2024, wakati wa ziara yake katika Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali jijini Dodoma, ambapo alijionea maendeleo ya ujenzi na ufungaji wa mitambo mipya ya uchapishaji wa nyaraka za serikali.

"Nyaraka nyingi muhimu huchapwa kwenye Gazeti la Serikali. Ni muhimu kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu namna ya kulipata gazeti hilo ili taarifa hizo ziwafikie kwa urahisi," amesema Waziri Lukuvi.

MAPENDEKEZO YA KUBORESHA UFIKIAJI WA NYARAKA ZA SERIKALI

Waziri Lukuvi alipendekeza jitihada maalum za kuhakikisha Gazeti la Serikali linapatikana mashuleni kwa njia ya kidigitali, kupitia mifumo ya kompyuta inayotumiwa katika elimu.

"Nitoe rai kwa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, hasa kwenye nyaraka ambazo ni za wazi, fanyeni uelimishaji ili wananchi waweze kufikiwa na taarifa za Serikali kwa urahisi," amefafanua.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa uwekezaji wa mitambo ya kisasa ya uchapishaji, akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha utunzaji wa nyaraka nyeti na kuongeza ufanisi wa kazi za Idara hiyo.

MABORESHO YA MIFUMO YA KIDIGITALI KATIKA IDARA YA MPIGA CHAPA MKUU

Kwa upande wake, Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, George Lugome, alisema kuwa Idara hiyo inatengeneza mfumo wa mtandao wa kidigitali utakaomrahisishia mteja kujaza taarifa na kufanya malipo ya matangazo yatakayochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

Hata hivyo, amefafanua kuwa mfumo huo hautahusisha taarifa za mirathi, kwani zinahitaji mhusika kuwasilisha vielelezo vyake vya uthibitisho kwa mujibu wa sheria.

Lugome aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa wa Serikali katika ununuzi wa mashine za kisasa utasaidia kuongeza uzalishaji wa nyaraka na kuongeza mapato ya Serikali.