Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, amesema kuwa atamwalika Rais Samia Suluhu Hassan, kushiriki katika sherehe kubwa ya Malkia wa Nguvu 2025, zitakazofanyika Aprili 04, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kusaga alitoa mwaliko huo usiku wa jana Machi 12, 2025, wakati wa uzinduzi wa msimu mpya wa Malkia wa Nguvu 2025, hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Msimu mpya unakuja na kauli mbiu ya "TWENDE DUNIANI", ambapo imebainishwa kuwa mwaka huu mashindano hayo yatafanyika katika kanda tano za Tanzania.
"Azma na maono yangu kwa miaka 30 iliyopita ni kuwa na jukwaa ambalo wanawake watahusika kwenye kila kitu ninachokifanya. Wazo la tuzo hizi lilianzia kwa mwanamke mjasiriamali aitwaye Mwanamakuka, na tuliona ni vyema kulifanya kuwa kubwa zaidi. Ndicho tunachosherehekea leo," alisema Kusaga.
Joseph Kusaga ameongeza kwa kusema "Tumeanzisha Redio mpya ya Wanawake tu iitwayo Malkia Choice FM, Hii ni sauti ya Wanawake.
"Sisi tunaamini wanawake ni bora sana duniani. Siku ya tarehe 04 Aprili 2025 tunamualika Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, najua anatusikiliza watoto wake, ili tusherehekee naye siku kubwa ya Malkia wa Nguvu jijini Dar es Salaam," aliongeza Kusaga.
Kwa mwaka huu, Tuzo za Malkia wa Nguvu 2025 zitafanyika katika kanda tano za Tanzania, ambazo ni:
📌 Kanda ya Ziwa
📌 Kanda ya Kati
📌Nyanda za Juu Kusini
📌 Kanda ya Kaskazini
📌Kanda ya Pwani
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED