Serikali: CEOrt-Roundtable kiungo muhimu mahusiano sekta binafsi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:15 PM Mar 14 2025
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Picha: Mpigapichga Wetu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Serikali imelisifu jukwaa la Wakurugenzi Watendaji (CEOrt -Roundtable) kwa kuendelea kuwa kiungo muhimu cha ushirikiano kati yake na sekta binafsi katika kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekta mbalimbali za maendeleo hapa nchini.

Akizungumza  wakati wa jukwaa la mazungumzo ya Iftar lililoandaliwa na CEOrt Roundtable lenye kauli mbiu ‘Maadili ya Biashara kwa Ukuaji Jumuishi’ katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam,  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema jukwaa hilo limeifanya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa karibu sana na sekta binafsi kuliko kipindi chochote kile kilichopita.

“Tunawapongeza sana CEOrt Roundtable kwa kushirikiana na serikali katika ajenda ya maendeleo ya nchi hii, mkiwa na mchango mkubwa katika kuajiri, kufanya maamuzi na kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yetu kupitia wanachama wenu,”

“Tunafurahia sana ushirikiano huu kati ya Serikali na Sekta binafsi na jitihada zinazoendelea kufanywa na CEOrt Roundtable katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu kupitia majukwaa mbalimbali na mafunzo,” amesema.

Pia ameisifu CEOrt Roundtable kwa kusaidia ukuaji wa uchumi na kuhimiza maadili ya kufanya biashara ambayo yanasaidia ukuaji wa biashara kwa kufuata maadili na uwazi unaohitajika katika jukwaa la kimataifa ili kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.

“Tanzania, kupitia taasisi mbalimbali kama vile Baraza la Biashara na kituo cha Uwekezaji imekuwa ikiweka mazingira bora ya kuvutia wawekezaji na miongoni mwa wawekezaji hao ni wanachama wa CEOrt Roundtable,”

“Hivyo, Wizara yangu itaendelea kuwashirikisha CEOrtRoundtable katika kupitia majukwaa mbalimbali ya ndani na nje ya nchi na nitafurahi kuona ushirikiano huu unakuwa zaidi,” amesema. 

Amelisifu jukwaa hilo kwa kuhimiza maadili na uwazi katika biashara ambapo kupitia amani na mazingira ya biashara yaliyopo nchini, wawekezaji wengi watavutiwa kufanya biashara nchini na kulipa kodi itakayoiwezesha Serikali kuhudumia wananchi na kujenga uchumi.

Naye Balozi John Ulanga ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje amesema wanachama wa CEOrt Roundtable wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata maadili ya kazi kama na kuhimiza uwajibikaji, akiitaka jamii kufanya biashara kwa uaminifu ili kuvutia wawekezaji zaidi.

Amesema Tanzania ni kitovu kizuri cha kufanya biashara katika Ukanda wote wa Kusini mwa  Jangwa la Sahara na Afrika, akiwataka wawekezaji kutumia amani na mazingiza mazuri ya biashara yaliyopo ili kutanua wigo wa biashara zao.

Wadau mbalimbali wakiwemo Mabalozi kutoka nchi za India, Uganda na maofisa kutoka idara mbalimbali za Serikali na wanachama wa CEOrt wameshiriki katika mazungumzo hayo yaliyohimiza uongozi wa kimaadili na uaminifu wa biashara katika kukuza imani, ustawi, na ustahimilivu wa kiuchumi wa muda mrefu wakati Tanzania ikitekeleza malengo ya maendeleo ya 2050.

Akitoa neno la shukran kwa Balozi Kombo, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt Santina Benson alisema wataendelea kufanya kazi na Serikali na wapo tayari kuendeleza ushirikiano uliopo.

CEOrt Roundtable iliyoanzishwa mwaka 2000 inayojumuisha Wakurugenzi Watendaji kutoka makampuni zaidi ya 200 kutoka sekta mbalimbali imekuwa na mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi, huku ikitoa mchango mkubwa katika kutoa ajira kupitia sekta binafsi na kuchangia takriban asilimia 40 ya mapato ya Serikali ya kodi  katika kusaidia ukuaji wa uchimi.