IMEZOELEKA kipindi cha mwezi huu Januari, kuna mambo magumu kwenye familia nyingi na sababu inaangukia kwenye matumizi makubwa, yakiwamo ambayo yasiyo rafiki nyumbani.
Matokeo yake, huwafanya wengine kupitia changamoto mbalimbali, kwa sababu ya mpangilio usio mzuri wa bajeti zao.
Baadhi ya wazazi wanafafanua jinsi mwezi wa kwanza unavyokuwa mgumu kwao. Hapo nina maoni ya Joyce Ngowi, mkazi wa Kimara, jijini Dar-es Salaam, anayeufafanua mwezi Januari, ugumu wake unawagusa baadhi ya watu wanaosafiri, wakitumia pesa kwa ajili ya nauli na hata wanapofika huko, wanaangukia bajeti nyingine kama kusaidia ndugu.
Akiendelea, akasema na wengine hufanya sherehe, ikiwamo kwa baadhi katika staili ya mjumuiko fulani na hilo linashuhudiwa sana mkoani Kilimanjaro, ikiwa mithili ya mila.
Kila ifikapo mwisho wa mwaka, huambatana na mengi, ikiwamo katika imani; sherehe kama za komonio.
Upande mwingine, ni tarehe zinasuburiana na ulipaji kodi za wapangaji vyumba, wanajikuta wanakopa, alimaliza kwa kusema watu wanapofika mwezi wa Januari wanatumia kulipa madeni na ada za shule kwa watoto, hivyo majumuisho yake ni kunaangukia mzigo wa changamoto.
Wazazi waliendelea kutoa changamoto zao, mkazi wa Bondeni, Dar-es Salaam (jina ninalo), ana yake ya kuainisha mwezi husika na changamoto aliyo nayo binafsi.
Anasimulia, mkewe kamwomba pesa za safari na zawadi kupeleka kwao kusalimia, lakini hilo limekuwa mzigo wa ziada kila anapotafakari shule zinafunguliwa, akiwa na uhitaji wa kumgharamia mwana anayesoma, anajikuta ana wakati mgumu.
Kama hilo, analo mzazi mwingine Pajrasi Hamadi, mkazi wa Goba, Dar es Salaam, akiutaja mwezi wa kwanza unakuwa mgumu kwake, kwa sababu ya bajeti za mwisho wa mwaka kuwa juu, wao wazazi wanakuwa na matumizi makubwa kipindi hicho.
Akaendelea kufafanua kwamba ni kipindi hata kwa kampuni nyingi, mauzo yake yanashuka, hivyo zinapata changamoto.
Mtazamo wa mzazi huyo ni kwamba, wao kada ya wazazi huangukia matumizi makubwa bila ya kuwa na akiba, zao lake wanaangukia kuyumba kiuchumi, ikiwamo katika mlo.
Mzazi mwingine, mkazi wa wilayani Kilombero, Morogoro asiyependa kutajwa jina gazetini, ana hoja ya kuwa ni kipindi cha kuanza kuandaa mashamba kwao wakulima, hivyo inawawia vigumu kumpatia mtoto mahitaji ya shule.
Akihitimisha kwa kuiomba serikali kuwawekea mkazo walimu, kuvumilia mapungufu ya watoto wakati huo.
Mzazi mwingine anayeishi Goba, Dar-es Salaam, mwenye mkazo mahususi katika ugumu wa kutatua ada za shule, pamoja na mahitaji yake kama vile sare, vifaa vya masomo, madaftari na begi la kiuanafunzi.
Mzazi huyo anajitambulisha kuwa na mtoto anayejiunga na kidato cha kwanza, mwingine yuko kidato cha tano, ada zao zote zinatakiwa mwezi huu.
Hilo analitaja kwamba limeendana na mengine ya kijamii, mwezi uliopita baadhi kawafanyia sherehe za kipaimara, zikiungana Krismasi, kwake mwenye kipato kidogo ikabaki mtihani mkubwa.
Ni bahati inabaki kuwa wajibu usiepukika, kuianzia ndani ya Sheria ya Mtoto na zinginezo zinazohusu ustawi wa jamii, ikiwamo Sheria ya Elimu.
Bila shaka ni vema wazazi wakajizatiti kwa vitu muhimu vya lazima kwa watoto wao kama vile elimu. Kibusara, kwa majukumu ya kijamii yaliyowazidi uzito wasigeuze nayo ya lazima, cha muhimu katika yote ni kupambania haki zao za msingi.
Tutakiane wote, Heri ya Mwaka Mpya, mapambano mema kwenye kuleta maendeleo!
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED