TLP imalize figisu kuna uchaguzi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:09 AM Jan 08 2025
TLP imalize figisu kuna uchaguzi.
Picha: Mtandao
TLP imalize figisu kuna uchaguzi.

NI zaidi ya miaka 2.5 tangu aliyekuwa mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, afariki dunia.

Lakini ni kama chama hicho kimeshindwa kupata mrithi wa nafasi hiyo, kutokana na mgogoro wa kiuongozi unaofukuta.

 Ndipo tunapojiuliza itakuwaje wakati uchaguzi mkuu unakaribia? Chama hiki kitashiriki au mambo ni yale yale?

 Mrema alifariki dunia mwishoni mwa Agosti mwaka 2022, lakini hadi sasa viongozi wamegawanyika makundi mawili wakiwamo wale anbao wanataka uchaguzi ufanyike na wengine wakipinga.
 
 Picha yenyewe iko hivi; baada ya kifo cha Mrema, Sekreterieti ya TLP ilimchagua mwenyekiti TLP  Zanzibar Hamad Mukadam,  kuwa Kaimu Mwenyekiti wa TLP Taifa.
 
 Mukadam alichaguliwa ili ashikilie nafasi hiyo kwa muda wakati chama kikiendelea na mchakato wa kufanya uchaguzi wa mwenyekiti wa chama taifa. Lakini hadi leo ni danadana na huku viongozi wakitishiana.
 
 Makundi yanayopingana ndani ya chama hicho ni lile linaloongozwa na  makamu Mwenyekiti wa Taifa, Dominatha Rwechungura na la Katibu Mkuu Richard Lyimo, linalopinga kufanyika kwa uchaguzi.
 
 Figisu zilianzia hapa, mara ya kwanza, chama kilipanga kufanya uchaguzi Januari 8 mwaka 2023, ukaahirishwa hadi Machi 6, 2023, lakini ukapigwa danadana hadi Mei mosi mwaka huo ukakwama tena.
  
 Baadaye ukapangwa kufanyika Desemba 28, mwaka huo, lakini haukufanyika, kisha ukapangwa kufanyika Januari 28 mwaka jana,  hata hivyo, ukaendelea kukapigwa kalenda hadi mwishoni mwa mwezi Juni.
 
 Hatimaye Juni 29, mwaka TLP chini ya Makamu Mwenyekiti Dominatha ikafanya uchaguzi uliomweka madarakani Ivan Maganza na timu yake, lakini ofisi ya Msajili wa Vyama  ikaibuka na kusema haiutambui.
 
 Kwa mujibu wa Dominatha, katika uchaguzi huo Maganza alichaguliwa kwa kura 35, huku wagombea wengine wa nafasi hiyo ya mwenyekiti wa taifa Kinanzaro Mwanga na Stanley Ndamugoba wakiwa na kura 10 kila mmoja, Richard Lyimo na Abuu Changaa wakiambulia sifuri.
 
 Hata hivyo, tangu wakati huo hadi sasa, viongozi hao hawajaingia ofisini kutokana na kile kinachoelezwa kuwa katibu mkuu ambaye nafasi yake ilichukuliwa na mwingine wakati wa uchaguzi anawazuia.
 
 Kwa figisu hizo za zaidi ya miaka miwili, nadhani ipo haja kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iingilie kati kumaliza mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama hicho ili kiweze kushiriki uchaguzi mkuu.
 
 Moja ya majukumu ya ofisi hiyo ni kulea vyama vya siasa, hivyo ingekuwa vyema akaziita pande mbili zinazopingana na kuziweka sawa ili chama kiweze kuendelea kufanya shughuli za kisiasa.
 
 Ninaamini katika mazingira ya sasa, si rahisi chama kushiriki uchaguzi au kuzunguka nchi nzima kujiimarisha wakati viongozi hawashirikiani na wanazuiana kuingia ofisi kwa sababu ya mgogoro wa kiuongozi.
 
 Julai mwaka jana, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilikaririwa na vyombo vya habari akitaka vyama hivyo kuepuka migogoro inayojitokeza kwa kuwa inaweza kuleta mifarakano katika taifa.
 
 Akakumbusha kuwa vyama vya siasa ni taasisi, hivyo vinapaswa kusajiliwa na kutenda majukumu yanayotambulika kidemokrasia na kuachana na vurugu zinazosababisha vyama hivyo kuwa na mpasuko.
 
 Kwa kuwa ofisi yake inatambua athari za migogoro katika vyama, ni vyema ikaingilia huo wa TLP ambao sasa una zaidi ya miaka miwili bila kupatiwa ufumbuzi na kusababisha chama kukosa mwenyekiti wa taifa.
 
 Uhai wa chama ni wanachama. Sidhani kwa mgogoro wa kiuongozi unaoendelea TLP chama hicho  kinaweza kuwa na wanachama hai na majasiri wanaoweza kusimama na kushindana kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

 Ipo haja ya ofisi hiyo ya msajili, wana TLP na wadau wapenda demokrasia kukinusuru ili jahazi lisiendelee kuzama na kuleta upweke kwenye harakati za siasa za vyama vingi.