TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Januari 27, kuhusu nishati na unatarajia kuridhia na kusaini mpango mahsusi wa nishati Afrika, kuidhinisha awamu ya kwanza ya Mipango ya Kitaifa ya Nishati kwa kipindi cha 2025 hadi 2030 na kupitisha tamko la Dar es Salaam.
Mambo hayo yatakayofanyika katika mkutano huo, yatasaidia kuweka ramani ya kimkakati kwa maendeleo ya nishati barani Afrika yenye lengo la kukuza upatikanaji wa nishati endelevu na ya haki kwa wote.
Nchi 14, ikiwamo Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria, Zambia na Senegal, zitashiriki katika mpango huo wa kuboresha upatikanaji wa nishati na uhakika wa umeme katika maeneo yao.
Tamko la Dar es Salaam litasaidia kuainisha maono ya pamoja ya Afrika kuhusu maendeleo ya nishati endelevu na litakuwa mwongozo wa kuendeleza nishati mbadala, kuboresha miundombinu na kuhakikisha usawa wa upatikanaji wa nishati barani kote.
Mkutano huo unalenga kuleta pamoja marais wa Afrika na wadau mbalimbali ili kuhamasisha mabadiliko katika sekta ya nishati barani Afrika na jumla ya watu 1,500 wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.
Mkakati wa nchi hizo kwa sasa ni kuja na mpango mahsusi ujulikanao kama ‘mission 300’ unaolenga kuweka mkazo kwenye kuharakisha matumizi ya nishati safi, endelevu na nafuu kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Mpango huo unalenga kupunguza pengo la upatikanaji wa umeme barani Afrika kwa kupanua miundombinu ya nishati katika maeneo ambayo hayajafikiwa.
Fahari ya Tanzania ni kuwa mwenyeji wa mkutano huo, kama kiongozi wa kuendeleza nishati mbadala barani Afrika.
Rais Samia Suluhu Hassan ameufanya uongozi wake wa kimkakati katika kuendeleza miradi ya nishati safi, na juhudi zake zimelifanya taifa kuwa mstari wa mbele kupigania nishati safi ya kupikia na suluhisho endelevu la umeme.
Juhudi za kidiplomasia za Rais Samia zimeiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee katika mazungumzo ya nishati barani Afrika.
Majadiliano ya mkutano huo yatagusia masuala muhimu ikiwamo maendeleo ya vyanzo vya nishati mbadala, upanuzi wa upatikanaji wa umeme vijijini na mijini na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya ya umma na mazingira.
Alisema, kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, Tanzania inalenga kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya kaya zinapata suluhisho la nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Tanzania katika kuongeza upatikanaji wa umeme vijijini, zaidi ya asilimia 99 ya vijiji sasa vina nishati hiyo, huku zaidi ya vitongoji 32,000 vikiwa vimeunganishwa na gridi ya taifa na mafanikio hayo yameleta maboresho makubwa katika sekta za afya, elimu na uchumi nchini, na kutoa msingi wa ukuaji zaidi.
Mkutano huo pia utatoa jukwaa kwa viongozi wa Afrika kutia saini makubaliano muhimu yatakayobadilisha mazingira ya nishati barani.
Hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuimarisha nafasi yake duniani na kuonesha maendeleo yanayofanyika katika sekta ya nishati.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kufikia Desemba 2024, uzalishaji wa umeme Tanzania bara ulikuwa umefikia megawati 3,169.20.
Pia, upatikanaji wa umeme uliongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi asilimia 78.4 mwaka 2020, kutokana na juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED